Habari za Kitaifa

Wataalamu wa nyumba za bei nafuu walilia Bunge walipwe

Na SAMUEL OWINO December 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Katika ombi lao waliloandika Novemba 27 2024, wataalamu hao waliotoa huduma za ushauri katika usimamizi wa ujenzi wa nyumba hizo sasa wanasema kucheleweshwa malipo yao kwa muda mrefu kunatishia kufaulu kwa mpango huo.

“Kucheleweshwa kwa malipo kwa muda mrefu kumesababisha matatizo ya kifedha yasiyostahili na dhiki ya kihisia kwa washauri walioathirika. Mgogoro huu unatishia utekelezaji mzuri wa mpango wa Nyumba za Bei Nafuu,” wanasema katika ombi hilo.

Ombi la chama cha Wasanifu Majengo Kenya (AAK) na chama cha Wakadiriaji Kiasi cha Kenya (IQSK) na Taasisi ya Wahandisi wa Kenya (IEK) limetiwa saini na Bw Karori Maina.

Wataalamu hao wanalitaka bunge kuelekeza idara ya Serikali ya Makazi na Ustawishaji wa Miji kukamilisha kandarasi zote za washauri hao na kurahisisha malipo hayo.

Aidha wanawataka wabunge kuingilia kati ili kuhakikisha kuwa madeni yote yanalipwa bila kuchelewa zaidi.

Walalamishi hao pia wamelitaka Bunge kuchunguza mgogoro kati ya maafisa wa idara ya nyumba ambao wanadai umeathiri kutolewa kwa malipo yao kwa wakati.

“Tunaomba bunge kwa unyenyekevu kuimarisha uwajibikaji na kurahisisha michakato ya utawala katika mpango wa nyumba za bei nafuu ili kuzuia masuala kama haya katika siku zijazo,” walalamishi waliwaomba wabunge.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan