Mazishi yaleta nuksi baada ya ukuta kuanguka na kuua waombolezaji watano Mombasa
WATU watano, miongoni mwao mwanamke mjamzito wameaga dunia baada ya ukuta kuanguka eneo la KCC Miritini, Mombasa, Jumatatu, Desemba 2, 2024.
Watano hao walikuwa wanahudhuria mazishi katika eneo hilo, na walikuwa wanapanga foleni kutazama mwili wakati mkasa huo ulipotokea.
Akithibitisha kisa hicho, Waziri wa Usafiri wa Kaunti ya Mombasa Dan Manyala alisema sehemu ya ukuta iliyobakia itamaliziwa kubomolewa.
“Watu watatu walifariki papo hapo huku wawili wakiaga dunia walipokuwa wanakimbizwa hospitalini. Mwanamke mmoja alikuwa mjamzito na alikuwa karibu kujifungua, kwa hivyo kihalisi tumepoteza watu sita,” akasema.
Bw Manyala alieleza kwamba mvua kubwa iliyodumu chini ya dakika 10 ilisababisha ukuta kuanguka na kuua, kujeruhi wakazi waliojikinga na mvua karibu na ukuta huo.
Mmoja wa walioshuhudia mkasa huo, Rashid Foya, ambaye ndiye mwenyekiti wa bodaboda eneo hilo, alisema ilichukua chini ya dakika mbili kwa ukuta huo wa futi tisa kuanguka.
“Mvua ilikuja na upepo mkali ambao uliangusha ukuta. Kulikuwa na watu waliokuwa wanajikinga na mvua karibu na ukuta, na upepo ulikuwa ukivuma kutoka upande mmoja,” alisema.
Kumekuwa kukinyesha mvua maeneo mengi Mombasa Jumamosi usiku huku mvua kubwa ila fupi ikishuhudiwa Jumatatu (leo).