Akili Mali

Ikiwa umekuza pamba nzuri na nyeupe ilete tutanunua pesa nzuri, kiwanda chatangaza

Na LAWRENCE ONGARO December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIWANDA cha kutengeneza nguo cha Thika, kimewahimiza wakulima hapa nchini kurejelea kilimo cha pamba kwa wingi.

Meneja wake mkuu wa maendeleo, Bw Hesbon Olweny’, alisema tayari wamezuru kaunti ya za Siaya, Homabay, Machakos,  na Busia kuwarai wakulima warejelee kilimo cha pamba kwa wingi.

Chini ya miaka miwili  sasa, kiwanda hicho kimetumia zaidi ya Sh70 milioni kwa kuinua kilimo cha pamba huku kikiwapa wakulima vifaa vya kilimo na mbegu za upanzi.

Meneja huyo amepongeza serikali kwa kuwa na ushirikiano wa karibu nao kwa kuhakikisha ukuzaji wa pamba umefufuliwa katika maeneo tofauti nchini.

Kiwanda hicho kinaendeleza kauli mbiu ya “Nunua Kenya, Jenga Kenya” ili Wakenya wazidi kununua bidhaa zao za hapa nchini na kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi ambazo zinalemaza viwanda vya humu nchini.

Wakulima wamehakikishiwa soko la haraka ambapo kiwanda hicho kiko tayari kununua pamba kuanzia Sh78 kwa kila kilo kutoka Sh52 za hapo awali.

Vilevile, kiwanda hicho kina mipango ya kufufua viwanda vya pamba vilivyofungwa hapo awali. Viwanda vya Madiany’ katika Kaunti ya Siaya na Luanda – Samia, Kaunti ya Busia ni kati ya vilivyofufuliwa.

Meneja huyo alieleza kuhusu ujio wa nguo za mitumba nchini ambayo ilisababisha viwanda vingi vya kushona nguo kufungwa hapa nchini.