Mashairi

MASHAIRI YETU: Mokua nimerudi

December 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

Hodi hodi washairi, mie mwenzenu nabisha.

Narudi tena kwa mori, moto moto nimewasha,

Tena nije kushauri, na ujumbe kuwapasha,

Nimerudi ukumbini,  niyatunge mashairi.

 

Siku nyingi kapotea, maisha yalinipiga,

Uchumi kanilemea, washairi kawaaga,

Na sasa nimerejea, washairi nawaiga,

Nimerudi ukumbini, niyatunge mashairi.

 

Naungana na wengine, niweze  kusadiana,

Kueneza kwa unene, lugha ilo na  dhamana,

Dunia sote tunene, Kiswahili kwa mapana,

Nimerudi ukumbini, niyatunge mashairi.

 

Isambae kwa haraka, mbio mbio kama moshi,

Ifikie wamerika, wachina wanakoishi,

Kote humu Afrika,  elimu lugha haishi

Nimerudi ukumbini, niyatunge mashairi.

 

Beti tano natamati, nimefika kileleni,

Mtiririko wa beti, nitatunga kwa makini,

Nitafunza kwa umati, iwangie akilini,

Nimerudi ukumbini, niyatunge mashairi.

HABIB MOKUA

OLJORAI , GILGIL

NAKURU

 

Ufisadi vyuoni

Tulo’dhani ni kidonda, limekuwa jinamizi,

Kwa hasira linavunda, lahitaji uganguzi,

Linatisha kama nunda, donda hili mmaizi,

Ufisadi ni asidi, hubabua vyuo vyetu.

 

Unaanza na behewa, kutafuna kama nyama,

Bila kubakisha hewa, husafisha kilo chema,

Kisha shina kuraruwa, kisalie kichelema,

Ufisadi pepo mbaya, hudumaza vyuo vyetu.

 

Latutia atiati, jitu hili ufisadi,

Yalo bora hatupati, kwa sababu ufisadi,

Si hayati si mamati, ya vyuo vyetu miradi,

Ufisadi ni ukoma, hulemaza vyuo vyetu.

 

Jaramogi hata sisi, imetuchapa bakora,

Walivamia fukusi, bilioni wakapora,

Vile vile kawa fisi, wakudumisha ukora,

Ufisadi domo tamu, watafuna vyuo vyetu.

 

Hongerani ile tume , fumbo hili kufumbua,

Tena wima msimame, wahusika kuwasua,

Ndo’ hili janga likome, vyuo vyetu kunasua,

Tutimue ufisadi, vyuo vyetu kuokoa.

AUSTINE O ONYANGO

MALENGA WA MTO NILE

CHUO KIKUU CHA JARAMOGI (JOOUST)

 

Ruto timiza ahadi

Rais Ruto naomba, telekeza  ulosema,

Ahadi ulizoamba, kutimiza ni lazima,

Mengi mambo umeamba,  popote ukituama,

Rais Ruto naomba, timiza uloahidi.

 

Mengi umetuahidi, hatamu lipochukua,

Tumesubiri kwa udi, ulosema kutimia,

Kukumbusha imebidi, miadi ulotupea,

Rais Ruto naomba, timiza uloahidi.

 

Ushuru lituahidi, tapungua tena sana,

Usalama kaahidi,  taboresha kwa mapana,

Kasema tajitahidi, bungeni uliponena,

Rais Ruto naomba, timiza uloahidi.

 

Elimu  juu nchini, yayumbayumba jamani,

Wahadhiri megomani, kote kote taifani,

Yaliyo Moi chuoni, yakata matumaini,

Rais Ruto naomba, timiza uloahidi.

 

Balozi takusifia, Kenya yetu kiboresha,

Kura nitakupigia, pasipo  kubabaisha,

Kwa sasa  nakuusia,  sera tata badilisha,

Rais Ruto naomba, timiza uloahidi.

EDWARD LOKIDOR 

“BALOZI WA KISWAHILI, TURKANA”

LODWAR

 

Akujuae

Mwana kaka dada njoni, babu bibi baba njoni,

Halafu mama mwiteni, mjomba sisahauni,

Na shangazi mfwateni, mkuje tujuzaneni,

Hakuna akujuae, zaidi yako mwenyewe.

 

Vile unavyojihisi, mamako hezi eleza,

Wala hakunae insi, awezae kukujuza,

Yani ni wewe halisi, ndie unajieleza,

Hakuna akujuae, zaidi yako mwenyewe.

 

Chochote ukiwazacho, ni nani akijuae,

Ama kile utakacho, ni nani akaguae,

Kilo ndani yako jicho, ni nani akionae,

Hakuna akujuae, zaidi yako mwenyewe.

 

Si mzazi si mwalimu, si mpenzi wala ndugu,

Mwenye kutaka kudumu, ni wewe wala si nugu,

Basi fanya si dhalimu, timiza zako abagu,

Hakuna akujuae, zaidi yako mwenyewe.

 

Malengo yako ng’ang’ana, mwishoni ukumbatie,

Kama vita we pigana, ndipo uje jishindie,

Basi mwana we pambana, usikuje ujutie,

Hakuna akujuae, zaidi yako mwenyewe.

JACOB NYAMAWI MWACHIRAMBA 

CHUO KIKUU CHA MURANG’A 

 

Asante Mungu

Nashukuru Maulana, kwa umbali nimefika,

Makubwa yalinibana, naweza kuyakumbuka,

Yale yasowezekana, kivyovyote elezeka,

Asante Mwenyezi Mungu, neema yako yatosha!

 

Njaa kaniondolea, lishe bora lipokosa,

Vyakula kanijalia, siha njema mimi sasa,

Elimu nilolilia, Jalali nakutakasa,

Asante Mwenyezi Mungu, neema yako yatosha!

 

Afya umenijalia, licha ya kuwa mgonjwa,

Damu ulokirimia, kanusurika magonjwa,

Kama siwe kuzuia, na kifo mi ningeonjwa,

Asante Mwenyezi Mungu, neema yako yatosha!

 

Ni wengi walotamani, kufika tulipofika,

Ndoto na kutimizeni, maisha yakajengeka,

Hawakuweza lakini, Izraeli kawapoka,

Nami nasema asante, neema yako yatosha!

 

Mungu unipe hekima, mwelekeo ulo sawa,

Zinifunike rehema, nikaishi sawasawa,

Na watu pasi na muma, nisije kaumbuliwa,

Usikie ombi langu, nataka neema yako!

 

Na tamati nimefika, kalamu naweka chini,

Nimelia kusikika, dua yangu masikini,

Maovu yanonifika, nepushe nayo Manani,

Pokea asante zangu, Mungu wangu nakuomba!

WINJOY GACHERI

(MTOTO WA MERU)

CHUO KIKUU CHA MLIMA KENYA

 

Msimu wa sherehe

Ni Desemba imefika, kama meli forodhani,

Mihemko na kuruka, ni furifuri densini,

mapochopocho twapika, yachacharika jikoni,

Ni msimu wa sherehe, ndugu yangu jihadhari,

 

Tunaenda vijijini, kuwasabahi wazee,

Naomba tuwe makini, na ajali tuzuie,

Dereva kule njiani,mtindi usitumie,

Ni msimu wa sherehe, ndugu yangu jihadhari,

 

Ukiwa burudanini, silewe kupindukia,

Linalotoka kinywani, liwe la kunyenyekea,

Sizue vita jamani, vitaweza kuumbua,

Ni msimu wa sherehe, ndugu yangu jihadhari,

 

Tarehe moja kifika, jiungeni ibadani,

Mola Aweze tukuka, shangwe zitoke vinywani,

Pia toeni sadaka, Mekulinda mwafulani,

Ni msimu wa sherehe, ndugu yangu jihadhari,

 

Muda wangu umefika, wa kuenda kijijini,

Tafurahi na kucheka, na wenzangu kijijini,

Gari letu laondoka, ni dereva usukani,

Ni msimu wa sherehe, ndugu yangu jihadhari,

SHEM BOSIRE,

MIGOMBA YA ZIWA KUU,

NYAMIRA

 

Paul Nyambane

Pachori ninakupaka, mavaziyo yanukiye,

Adhimu kama baraka, moyoni ufurahiye,

Derea bila kuchoka, ndotoyo ikatimiye,

Ruka juu ukitaka, uwe unashangiliya,

 

Ilahi mola Rabuka, akubariki daima,

Pepa kwako ninatema, bingwa Paul Nyambane,

Allah Mola Karima, daima ndiye mnene,

U-tukufu juu sema, mtukuze mara nne,

 

Lahiki zake baraka, zije kwako lakilaki,

Neema kwako itoshe, ilojawa wema wake,

Yailahi akuvushe, mbali sana ukafike,

Aliyati akulishe, ili usiwe mpweke,

 

Mjasiri nakujua, kwa kukemea mapepo,

Bananga nguvu za giza, unapotamka bwana,

Awe Mola muweza, Muumba mwenye thamana,

Ndiye atakuongoza, usafiri kama jana,

Ejema kwake Hallaku, twaa dua la maana,

HENRY MOINDI MONG’ARE

MGANGA WA MISTARI

NYAMIRA-KENYA-(046)

 

Maisha kutafuta!

Usione nasinzia, usemayo nasikia,

Na tena nakuambia, utakuja kujutia,

Ni wapi nilikosea?, hukomi  kuniongea,

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana!

 

Unajifanya rafiki, kumbe wewe ni nafiki,

Kila siku ni mikiki, kusababishia dhiki,

Hakika huambiliki, na tena husemezeki,

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana!

 

Sumu yako waitema, ewe joka la mdimu,

Majirani walalama, umekosa umuhimu,

Wasubiri ya kiama, uangamie  kuzimu,

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana!

 

Uvumi unaeneza, kuhusu yangu maisha,

Wasahau kujikaza, mikasa wasababisha,

Aushini wateleza, kujipandishia presha,

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana!

 

Kila siku ni umbeya, na fitina kutafuta,

Kunitakia mabaya, kuanzisha nazo vita,

Hauoni hata haya, vikaoni umekita,

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana!

 

Ila sasa nakuonya, itabidi unikome,

Mimi tena nakukanya, mdomoni uniteme,

Ukizidi takufinya, ukimbilie mahame,

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana!

 

Kadi tama nimefika, nimesema ya moyoni,

Wambeya nikiwashika, nitawabonda usoni,

Tuepuke pandashuka, tujikaze maishani,

Maisha ni kutafuta, na sio kutafutana!

KAKA KULE,

AUGUSTINE KULECHO,

LUKHUNA-TONGAREN 

 

Noma ya NTV

Wino huu nawapia, na kusema Noma pia,

Filamu hii yapia, NTV ilokuja Nia,

Kuelimika hi njia, ya maisha na kutia,

Twendeni NTV fikia, kwa umarufu kwapia.

 

Saa mbili zakujia,usiku umetulia,

Na ufikapo kimbia, kufungua angalia,

Kipindi kusimulia, yaloandaliwa tia,

Twendeni NTV fikia, kwa umarufu kwapia.

 

Na kunuku kwa hisia, ili kuwa historia,

Kwa jamii yako njia, bora nayo kupitia,

Na kuwa yakuvutia, kwayo uloyapitia,

Twendeni NTV fikia, kwa umarufu kwapia.

 

Tamati ndo nafikia,usipitwe wewe pia,

Shikilia yalojia, kupata yalokimbia,

Kwa hiyo na familia,kuanza mwanzo wa njia,

Twendeni NTV fikia, kwa umarufu kwapia.

EDWARD AMANI MGHANGA

WERUGHA BASIC

TAITA TAVETA COUNTY