Tuwaige Watanzania kwa kupunguzia viongozi askari
KENYA ni nchi ya ajabu sana. Wanaitaja kuwa kati ya mataifa ya tatu ulimwenguni ama tuseme yanayoendelea japo lina unafiki mkubwa. Je wabunge wanahitaji askari kuwalinda?
Wasinisikie waheshimiwa, watadhani nimepandwa mahoka. Katika nchi jirani ya Tanzania wabunge wana askari wa kuwalinda? La.
Nimebahatika kuwa na rafiki zangu wabunge na pia mawaziri wa Tanzania na wanashangaa ghaya tunavyotumia rasilimali za umma kuwalinda watu na mali yao binafsi.
Tanzania, mawaziri wakiwa katika shughuli zao hutampata polisi katika msafara wake. Wabunge nao hawajui hizo habari.
Mawaziri wanaenda kilabu na hata kuwatumbuiza wapiga sherehe na kuingia gari lake anapopiga mafuta hadi kwake kama ni Mikocheni B ama Kawe na hakuna atakayemsumbua.
Hapa Kenya yetu tukufu, kitovu cha demokrasia na katiba endelevu hata mwakilishi wadi yuataka mlinzi. Acha tufanye hesabu rahisi. Kenya ina wabunge 349 katika bunge la taifa, kila mmoja ana polisi mlinzi wake.
Spika ana askari wake watiifu karibu watano naibu spika ambaye ni mbunge ana zaidi ya askari mmoja.
Katika bunge la seneti, kuna maseneta 67 na spika wao. Sikwambii hizi afisi zisizoeleweka sana za Viongozi wa Wengi na Wachache. Wanalindwa kama mboni ya jicho.
Sasa askari zaidi ya 500 kuwalinda watu afisini na kuchunga mtu asiwaibie usingizi kwao!
Ndiyo Kenya yetu hiyo, wakuu wasomaji wangu.Wakuu wa mashirika ya umma wana walinzi pia, wanazidi 200.
Si hayo tu, katika idara ya mahakama kuanzia kwa hakimu hadi jaji mkuu. Ikumbukwe kuwa hawa wanalipwa mshahara kuwa polisi na marurupu ya kuwalinda wakubwa wao.
Hata kuna wakurugenzi wa idara tofauti ambao wana walinzi. Msururu mwingine wa viumbe hawa wanaolindwa ni magavana na manaibu wao. Wana polisi kazini na nyumbani.
Kuna sehemu nyingi za Kenya zinahitaji huduma za polisi hata tu katika jiji kuu la Nairobi.
Katika maeneo ya kaskazini mwa nchi polisi ni kiungo muhimu kukabiliana na tishio la ugaidi. Badala ya kutumwa wawasaidie wenzao mipakani, utawapata katika eneo la mapokezi kwa waziri ama mbunge wakizunguka kwa viti na kusubiri amri.
Wamefanywa kuwa taarishi. Wametumiwa vibaya kwa muda mrefu. Wanasaidiana na washiriki wa wakubwa kuchukua orodha ya kuwaona na kupanga miadi.
Wakati mwingine hawa askari wanajipata wakiwabebea wakuu wao mikoba, vipochi na vipatakalishi kabla ya kusoma hotuba. Ndiyo Kenya yetu hiyo.
Nimegusa tu sehemu moja.
Tanzania, wanaopata walinzi na si lukuki ni rais, makamu wake na spika. Wengine watangamane ovyo na raia.
Inawezekana ujamaa uliwasaidia na kila mtu akamchukua mwenzake kuwa ndugu. Hawana wakati wa kuvamiana. Viongozi wanajua jukumu lao ni kutekeleza masilahi ya umma.
Paul Nabiswa ni mhariri wa NTV