Sudi, Aladwa wangali ‘bubu’ bungeni kwa miaka miwili mfululizo
KWA mara nyingine Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na mwenzake wa Makadara George Aladwa ni miongoni mwa wabunge 19 ambao hawajatamka lolote bungeni mwaka huu, ripoti moja imefichua.
Bw Sudi ni mwandani wa karibu wa Rais William Ruto, ambaye ndiye kiongozi wa chama tawala United Democratic Alliance (UDA) huku Aladwa akiwa mshirika wa karibu wa kiongozi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Kwenye ripoti kuhusu utendakazi wa wabunge iliyotolewa na shirika la Mzalendo Trust wabunge wengine “bubu” ni pamoja na; Mathias Robi (Kuria Magharibi, UDA), Charles Gimose (Hamisi, ANC), Joseph Tonui (Kuresoi Kusini, UDA), Samuel Gachobe (Subukia, UDA), Paul Abuor (Rongo, ODM) na Mbunge wa Bahati Irene Njoki (Jubilee).
Wengine ambao hawajatoa mchango wowote kwa hoja au miswada bungeni ni; Irene Kasalu (Mbunge Mwakilishi wa Kitui, Wiper), Patrick Simiyu (Cherangany, DAP-K), Paul Chebor (Rongai, UDA), Stephen Karani Wachira (Laikipia Magharibi, UDA), Mohamed Soud Machele (Mvita, ODM), Afred Mutai (Kuresoi Kaskazini, UDA), Clement Sloya (Sabatia, ANC) na Barre Hussein Abdi (Tarbaj, UDA).
Wabunge maalum; Dana Joseph Hamisi (ANC) na Joseph Wainaina wa UDA pia hawajasema lolote kwenye kikao cha bunge lote mwaka huu.
Akitoa ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mzalendo Trust Caroline Gaita alisema licha ya wabunge hawa hupigia kura miswada muhimu kama vile ile inayohusu afya, nyumba na utozaji ushuru.
“Vile vile, wabunge hawa walishirikia upigaji kura kuhusu mswada wa kumwondoa afisini aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Oktoba 8, 2024,” anaeleza.
Kulingana na ripoti ya hiyo ya Mzalendo Trust, shirika linalofuatilia utendakazi wa wabunge, wabunge waliondokea kuwa wachapa kazi zaidi ni; Wilberforce Oundo (Funyula, ODM), Betrice Elachi (Dagoretti Kaskazini, ODM), James Nyikal (Kisumu Mashambani, ODM), Makali Mulu (Kitui ya Kati, Wiper) na Adan Keynan (Eldas, Jubilee).
“Wabunge hawa walichangia mara nyingi, hoja na miswada ukumbini kando na kushiriki upigaji kura kwa hoja na miswada muhimu,” Bi Gaita akaeleza.
Katika Seneti, uchunguzi wa Mzalendo Trust ulibaini kuwa maseneta wazembe ni pamoja na Issa Boy Juma (Kwale, ODM) na maseneta maalum Betty Batuli (UDA) na Shakilla Mohamed (Wiper).
“Watatu hao wote hawakuwepo wakati wa upigaji kura kuhusu miswada mitano muhimu. Miswada hiyo ni pamoja na Mswada wa Nyumba za Gharama Nafuu 2024, Mswada kuhusu Afya ya Kimsingi, 2024, Mswada kuhusu Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF), Mswada wa Sukari na Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC ya 2024,” Bi Gaita akaeleza.
Maseneta walioorodheshwa kama wachapa kazi zaidi ni; Samson Cherargei (Nandi, UDA), Eddy Oketch (Migori, ODM), Tabitha Mutinda (Seneta Maalum, UDA), Erick Okong’o O’Mogeni (Nyamira, ODM) na Seneta maalum Gloria Orwoba (UDA).
Kulingana na ripoti hiyo, Seneta maalum Crystal Asige na Bw Cherargei ndio wanaoogozwa kwa kudhamini miswada mingi katika Seneti—sita na tano, mtawalia.
Katika Bunge la Kitaifa Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa na mwenzake wa Suna Magharibi Peter Masara ndio wanaoongoza kwa kudhamini miswada minne na mitano, mtawalia.
Mzalendo Trust hufuatilia utendakazi wa wabunge kwenye ukumbi wa mijadala pekee wala sio katika kamati za bunge au katika maeneo bunge yao.
Ripoti ya hivi punde imetolewa siku mbili baada ya Bunge la Kitaifa kuahirisha vikao vyake vya kawaida kwa siku kuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Vikao hivyo vitarejelewa Jumanne alasiri Februari 11, 2025.