Makala

UCHAMBUZI: Kina nani wanapigana Syria na kwa nini?

Na REUTERS December 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

TUKIO la waasi wa Syria kuteka na kulitwaa jiji kuu la Damascus na kupelekea Rais Bashar Al-Assad kuyoyomea kusikojulikana kufikia wakati wa kupeperusha habari hii, limeshtukiza dunia ambayo kwa miaka ya hivi karibuni ilikuwa imesahau kuhusu vita nchini humo.

Ni tukio ambalo litakuwa na athari kwa nchi hiyo na nje ya mipaka yake.

Ni nini kinaendelea?

Waasi hawa walianzisha mashambalizi ya kushtukiza mnamo Novemba 26, 2024 wakilenga maeneo ya Kaskazini na Kaskazini Magharibi ya Aleppo.

Na kufikia Novemba 29 na 30, walifaulu kuingia jijini kisha wakawafurusha wanajeshi wa serikali.

Ni mara ya kwanza uongozi wa jiji hilo umebadilika tangu 2016. Wakati huo, majeshi ya serikali yalishinda waasi ambao walikuwa wanatawala Wilaya za Mashariki jijini Aleppo. Wanajeshi hawa walipigwa jeki na majeshi ya Urusi na Iran.

Waasi hao wameingia hadi maeneo ya Kusini na Kusini Magharibi mwa Aleppo huku wakiteka himaya ya mkoa wa Hama.

Serikali imeapa kujibu mashambulizi haya. Itakumbukwa kuwa Urusi ilimwaga wanajeshi wake wa angani nchini Syria kusaidia Assad mnamo 2015.

Pia sasa, Urusi imetuma wanajeshi ambao wanaendeleza mashambulizi ya angani kusaidia jeshi la Rais Assad.

Tukio hili linaashiria kuwa hali imekuwa mbaya sana. Kabla ya hili kujiri, vita vilikuwa vimetulia lakini sasa hali ya hatari imerejea. Maafa yamepanda hadi mamia ya maelfu tangu 2011 wakati vita vilichipuka kupinga utawala wa Assad.

Kufikia sasa, zaidi ya nusu ya raia waliokuwa kabla ya vita kuanza (milioni 23) wamelazimika kutoroka makwao, huku mamilioni wakihamia nchi nyingine wakiwa wakimbizi.

Hawa waasi ni kina nani?

Mashambulizi yalianzishwa na wanamgambo wa Hayat Tahrir al-Sham (HTS) awali wakiitwa Nusra Front.

Kundi hili lilikuwa tawi mojawapo la al-Qaeda katika vita vya Syria kabla ya kutengana 2016.

HTS inaongozwa na Abu Mohammad Al-Golani na ni kundi la waasi wenye ushawishi mkubwa sana katika ukanda wa Idlib.

Eneo la Idlib liko Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo na HTS wametawala hapa licha ya Rais Assad kushinda vita katika maeneo mengine.

Amerika, Urusi, Uturuki na nchi nyingine zimeorodhesha HTS kama  kundi la kigaidi.

Waasi wengine wanaopinga HTS wameanzisha mashambulizi tofauti kutoka maeneo yaliyo kaskazini mwa Aleppo. Waasi hawa wanapigwa jeki na Uturuki na wameshirikiana na Jeshi la Kitaifa la Syria (Syria National Army).

Kwa nini vita vya Syria vimeshika moto sasa?

Licha ya Syria kukosa amani, vita vimepungua bila kubadilika kwa maeneo ambayo yanadhibitiwa na serikali na waasi kwa miaka mingi. Nchi hii imegawanywa katika maeneo tofauti ambapo kuna vikosi vya wanajeshi wa nchi za kigeni.

Urusi na Iran zina ushawishi mkubwa katika maeneo ambayo yanaongozwa na serikali ya Syria. Hii ndiyo sehemu kubwa ya Syria na wanajeshi wa nchi hizi, wanapiga jeki serikali ya Rais Assad.

Vile vile, Amerika ina vikosi vya wanajeshi Kaskazini Mashariki na Mashariki mwa Syria. Wanasaidia Jeshi la Demokrasia ya Syria (Syrian Democratic Forces) ambalo linaongozwa na Wakurdi.

Pia, Uturuki ina kambi za jeshi katika eneo linaloongozwa na waasi Kaskazini Magharibi. Msaada wa kivita kwa Syria umeathiriwa na vita kati ya Israeli na Iran, pamoja na makundi ya kivita yanayosaidiwa na Iran.

Wanamgambo wa Hezbollah wamelemewa katika vita vya miezi miwili dhidi ya Israeli nchini Lebanon.

Hezbollah, ambayo ilimsaidia Rais Assad kurejesha udhibiti wa Aleppo 2016, ilikubali kusitisha vita na Israeli wiki iliyopita.

Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Amerika, Jake Sullivan, aliambia Shirika la habari la CNN kuwa waasi walipata fursa ya kuwa na nguvu zaidi kwa sababu nchi zinazosaidia Syria zilijukumika zaidi kijeshi katika nchi nyingine.

Alisema migogoro mingi ya kikanda inayohusisha Urusi, Ukraine, Israel, Lebanon na Iran inaweza kupoteza makini ya nchi hizi na kuwapa waasi nguvu ya kushambulia.

Makubaliano kati ya Urusi na Uturuki yamefanya hali kuwa shwari katika eneo la Kaskazini Magharibi tangu mwaka 2020.

Lakini Uturuki imesikitishwa na Rais Assad kukosa kukumbatia mwafaka na upinzani ili kumaliza mzozo huo.

Maafisa wa Uturuki wanateta kwa sababu wao wanajaribu kuzuia makundi ya waasi kushambulia, lakini vikosi vya Syria vinashambulia waasi.

Waziri wa mashauri ya kigeni Uturuki, Hakan Fidan, anataka Rais Assad na waasi waafikiane ili kuzima mgogoro.

Uturuki ina hofu kubwa kuhusu ushawishi wa makundi yanayoongozwa na Wakurdi, ambao ni washirika wa Amerika lakini wanaonekana kuwa magaidi na Uturuki.

Shirika la habari la Uturuki, Anadolu, liliripoti kuwa kundi hili la waasi (Syrian National Army) liliteka mji wa Tel Rifaat na kuwapokonya wanamgambo wa Kikurdi wa YPG.

Wakati huo huo, Urusi na Iran zimekariri kuunga mkono serikali ya Syria.

Kuna mpango wa kuwa na amani?

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio 2015 likilenga kumaliza mzozo huo.

Baraza hili linashinikiza kuwepo kwa Katiba mpya, uchaguzi unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa, na utawala wa uwazi na uwajibikaji. Azimio hili bado halijatekelezwa.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Geir Pedersen, alisema kuendelea kwa vita hivi kunaashiria kufeli kwa juhudi za washikadau mbalimbali kuangazia mzozo huu.

IMETAFSIRIWA NA LABAAN SHABAAN