Natilia shaka urafiki wa mke wangu na pasta
Mke wangu ana uhusiano wa karibu sana na pasta wake ambao nahisi umekiuka mipaka. Pasta amekuwa akija nyumbani na kukaa hadi usiku. Hata akishaondoka bado wanaendelea kuchati kwa simu hadi usiku wa manane.
Hiyo ni kukosa heshima. Itabidi usimame imara ukanye mkeo pamoja na huyo pasta kuhusu tabia hii. Ikiwezekana mwambie mwenzako kwamba hutaki aendelee na uhusiano huo.
Anadai hajaoa, vitendo vinaonyesha tofauti
Nimekuwa katika uhusiano na jamaa ambaye anadai hana mke ila namshuku. Hajawahi kuniruhusu nimtembelee kwake. Pili, usiku hashiki simu wala kujibu SMS kwa wakati. Tatu, tukikutana wikendi ni saa chache tu. Kisha ameniambia Krismasi hii hatutaonana. Ana mke?
Ukweli ni kwamba hizo ni ishara tosha za mtu aliye na mke au yupo kwenye uhusiano thabiti.
Nimerejea toka ng’ambo nikapata ameolewa
Miaka 5 iliyopita nilienda majuu kwa masomo nikaacha mchumba wangu hapa. Pandashuka za maisha zikawa nyingi hata nikafifia katika mawasiliano naye. Nilirudi nyumbani wiki iliyopita nikapata ameolewa. Ni haki?
Kamwe huwezi kumlaumu. Umeungama kwamba ulikaa miaka mingi na pia ukazima mawasiliano naye. Si haki kwako kupotea muda huo wote kisha utarajie binti angekaa tu na kukusubiri.
Tunapendana ila wazazi wake hawanitaki
Kwa miezi kadhaa nimekuwa katika uhusiano na kaka fulani na hata tumeshatambulishana kwa wazazi. Lakini wazazi wake hawanitaki kabisa, hata wanajaribu kuvunja uhusiano wetu. Nifanyeje?
Mapenzi ni baina ya watu wawili na hivyo uamuzi ni wako na mwenzio. Lakini pia ni vyema kupata baraka za wazazi. Ni wajibu wa jamaa kuzungumza na wazazi wake kuhusu uhusiano wenu ili kuondoa tetesi zilizopo.