Wakazi katika kaunti wasusia Jamhuri Dei wakitaja kuyeyuka kwa uzalendo wa viongozi
WAKAZI katika kaunti nyingi walisusia hafla za Sikukuu ya Jamhuri ambazo maafisa walisoma hotuba ya Rais William Ruto.
Hata hivyo, hakukuwa na matukio ya kuzomewa kwa maafisa hao.
Mjini Nyeri, sherehe hizo katika uwanja wa Dedan Kimathi zilihudhuriwa na watu wachache huku wengi wakiwa ni watoto waliovutiwa na soda na mikate iliyotolewa bila malipo.
Gavana Mutahi Kahiga na maafisa wa serikali ya kaunti yake walisusia hafla hiyo iliyosimamiwa na kamishna wa kaunti hiyo na naibu wake.
Wanasiasa wa eneo hilo wakiwemo wabunge na madiwani pia hawakuhudhuria.
Katika Kaunti ya Embu, hata hivyo, sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mbui Njeru, Runyenjes ziliongozwa na gavana Cecily Mbarire.
Bi Mbarire alisema wakazi 127,000 wa Embu wamejiandikisha kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii, (SHA).
Katika Kaunti ya Laikipia, sherehe hizo zilifanyika katika Shule ya Msingi ya Kinamba GG, Laikipia Magharibi.
Gavana Joshua Irungu aliungana na Kamishna wa Kaunti Onesmus Kyatha katika hafla ambayo wanasiasa waliepuka.
Nairobi, vijana 900 katika Kaunti-ndogo ya Starehe walioajiriwa na serikali kusafisha kingo za mto Ngong walisafirishwa kwa mabasi saa kumi na mbili asubuhi ili kuhudhuria Sherehe za Jamhuri Dei katika bustani ya Uhuru Gardens.
Wakazi wa Uasin Gishu walitaja ukosefu wa uzalendo miongoni mwa viongozi kuwa chanzo kikubwa cha idadi ndogo kuhudhuria sherehe za Jamhuri Dei Jijini Eldoret.
Wakizungumza Eldoret walisema sherehe hizo zimekosa ladha siku hizi kutokana na tabia ya viongozi kukosa uzalendo na kutojali wananchi wa chini.
“Siku hizi Wakenya wengi hawana imani na viongozi ambao hawana uzalendo kwa watu ambao wanawaongoza,kuna haja ya viongozi kurudi kwa mizizi na kukumbatia uzalendo ili kuvutia wananchi wengi,” alisema Sheikh Abubakar Bini kiongozi wa CIPK, North Rift.
Laikipia Mashariki, Naibu Kamishna wa Kaunti Patrick Muli aliongoza sherehe hizo katika Shule ya Msingi ya Ndemu ambazo zilikosa idadi ya kutosha.
Sherehe za Kajiado zilifanyika katika uwanja wa Oloitip tip, Loitoktok, Kajiado Kusini.Gavana wa Kajiado, Joseph Lenku, alisema nchi iko katika njiapanda bila IEBC.
Seneta wa Kajiado, Samuel Seki, aliradidi wito huo.
Na Mercy Mwende, George Munene, Titus Ominde, Stanley Ngotho, Mwangi Ndirangu na Sammy Kimatu.