Jinsi Ruto anavyong’ang’ana kurejesha imani katika utawala wake
RAIS William Ruto anaonekana yu mbioni kurejesha imani ya wakosoaji wa serikali yake wakati huu ambapo umaarufu wake umedororoa machoni pa Wakenya wengi.
Siku mbili baada ya kukutana na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Jumatano Desemba 11, 2024, Rais alikutana na viongozi wa makanisa ya Kievanjelisti na Kipentekosti.
Mnamo Jumatatu, Desemba 9, 2024, Dkt Ruto alisafiri hado kijiji cha Ichaweri, Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu, alikokutana na Bw Kenyatta. Japo, ilisemekana kuwa mkutano huo ulilelenga kupalilia umoja wa kitaifa, wadadisi wanasema mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Dkt Ruto kutuliza wakazi wa Mlima Kenya kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hata hivyo, Bw Gachagua amepuuzilia mbali hatua hiyo akisema itaambulia patupu kwani “watu wa Mlima hawakubali kurudi Misri”.
Jumatano, ilianza juhudi za kurejesha imani ya serikali yake kwa asasi ya kanisa kwa kukutana na viongozi makanisa ya Kievanjelisti na Kipentekosti katika Ikulu ya Nairobi; wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Deliverance Kepha Omae.
Mkutano huo unajiri baada ya kuibuka kile kilichotajwa kama uhasama kati ya baadhi ya viongozi wa makanisa na utawala huu kuhusu sera zake zisizofaidi raia wa kawaida na maovu mengine.
Kwa mfano, mnamo Oktoba 21, mwaka huu, Kasisi Teresia Wairimu, ambaye ni mwanzilishi wa Kanisa la Faith Evangelistic Ministries (FEM) alimkosoa Rais Ruto na utawala wake.
Alitaja maovu serikalini kama vile ufisadi, ukiukaji wa haki za kibinadamu kama sababu inayoashirikia kuwa taifa linaelekea mkondo mbaya chini ya uongozi wa Dkt Ruto.
“Kama mpiga kura aliyeichagua serikali hii, nimeaibika pakubwa,” Kasisi Wairimu akasema wakati wa ibada ya Jumapili.
Kanda ya video iliyomwonyesha kasisi huyo akiishambulia serikali ya Rais Ruto kwa maneno makali iliibua msisimko mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kanda nyingine ya Kasisi Tony Kiama wa Kanisa la River of God ilisambaa kwa kasi mitandaoni Novemba baada ya Kiama kuishambulia serikali ya Ruto akisema “haiendelezi matakwa ya Mungu bali yale ya shetani.”
Kasisi huyo alitaja mauaji ya waandamanaji wakipinga Mswada wa Fedha wa 2024 mnamo Juni mwaka huu, kupanda kwa gharama ya maisha na ufisadi serikali kama ithibati kwamba “serikali inatumikia matakwa ya shetani.”
Lakini ukosoaji mkali wa serikali ya Rais Ruto ulitoka kwa Maskofu wa Kanisa Katoliki mnamo Novemba 14, 2024. Ulisheheni uzito mkali kutokana na heshima na ushawishi wa maaskofu wa Kanisa hilo lenye idadi kubwa ya waumini nchini Kenya.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB) Askofu Mkuu Maurice Muhatia, waliishutumu serikali ya Dkt Ruto kwa kuendeleza “mienendo ya kutoa kauli za uwongo,” na kufeli kutimiza ahadi ilizotoa wakati wa kampeni.
“Kimsingi, inaonekana kuwa ukweli haupo na kama upo, ni yale serikali inasema,” baraza la KCCB likasema kwenye taarifa.
Maskofu hao walikemea ufisadi, ulafi na viwango vya juu vya ushuru unaodumaza ukuaji wa uchumi.
Isitoshe, mwezi jana, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nairobi Philip Anyolo aliamuru kurejeshwa kwa Sh2.8 milioni ambazo Rais Ruto alitoa kama “sadaka” kwa Kanisa Katoliki la Soweto, eneo bunge la Embakasi Mashariki.
Lakini Jumatano, Rais Ruto alionekana kunyoosha mkono wa maridhiano na makanisa alitaja mashirika ya kidini kama washirika wakuu katika kuendeleza uwiano wa kitaifa.
“Makanisa na mashirika mengine ya kidini kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine huhudumia watu wale wale. Na asasi hizi zimefanya kazi pamoja kuendeleza uwiano wa kitaifa na utoaji wa huduma muhimu kama za kiafya, kielimu na kuwasaidia wasiojiweza katika jamii. Tunajitolea kudumisha ushirikiano huu,” Rais Ruto akasema kwenye taarifa baada ya kukutana na viongozi hao wa kidini.
Itakumbukwa kuwa wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 viongozi wa makanisa ya Kievangelisti na Kipentekosti walikuwa mstari wa mbele kumfanyia kampeni Rais Ruto. Inaaminika kuwa baadhi yao waliwashawishi waumini wao wampigie kura Dkt Ruto na kumwezesha kumshinda mgombeaji wa Azimio Raila Odinga.
Licha ya kukosolewa na viongozi wa kidini mwaka huu, Rais Ruto amesimama kidete akishikilia kuwa serikali yake itaendelea kushirikiana na makanisa inapowahudumia Wakenya.
Aidha, licha ya mwenendo wake wa kutoa michango ya fedha kwa ajili ya miradi ya makanisa kukosolewa, Rais Ruto ameshikilia kuwa ataendelea kutoa michango hiyo “kwa sababu nimekuwa nikifanya hivyo kwa miaka 30 iliyopita”.