Makala

Waboni wanavyotaabika kupata elimu ya chekechea

January 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na Kalume Kazungu

MATUMAINI ya watoto wa jamii ya walio wachache ya Waboni kupata elimu yanazidi kufifia, kufuatia hatua ya hivi punde ya serikali ya kaunti ya Lamu kufunga shule zote za chekechea ambazo zimekuwa zikihudumia watoto hao.

Shule tano za msingi za Wadi ya Basuba, ikiwemo Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe zilifungwa tangu 2014 kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyokuwa yakitekelezwa na Al-Shabaab.

Mnamo 2015, serikali kuu iliafikia kuzifungua shule hizo na kutuma walimu 10 eneo hilo.

Aidha kufunguliwa kwake kulikuwa kwa muda tu kwani baadaye walimu wote walitoroka kwa kuhofia kushambuliwa na Al-Shabaab.

Shule hizo hadi sasa zimebakia kuwa mahame.

Aidha mwaka huu, shule hizo za chekechea hazijafunguliwa tena baada ya kaunti kudai kwamba walimu waliokuwa wakihudumu waliajiriwa kwa kandarasi na kwamba kandarasi hiyo ilikuwa imefikia ukingoni.

Katika kikao na wanahabari mjini Lamu mwishoni mwa juma. Wawakilishi wa jamii ya Waboni walieleza kusikitishwa kwao na hatua ya kaunti kukosa kutuma walimu wa kuendeleza vituo hivyo vya chekechea.

Bw Abdalla Salale alisema inahuzunisha kuona kwamba watoto wengi wa jamii ya Waboni ambao wamefikisha umri wa kwenda shule wamebaki kurandaranda mitaani bila elimu.

Bw Salale alisema hali hiyo imewatia hofu kwani huenda wanafunzi hasa wale wa kike wakaishia kutungwa mimba mitaani kwa kukosa elimu.

Waliitaka kaunti kuhakikisha walimu wa kutosha wa ECDE wanaajiriwa ili kuendeleza masomo hayo eneo hilo.

“Matumanini yetu yalikuwa kwa hizi shule za ECD. Angalau watoto wetu wadogo walikuwa wakijiunga na shule hizi kupata masomo. Tunasikitika kwamba hivyo vituo vya ECDE pia vimefungwa kwa wakati huu. Watoto wetu wamebaki majumbani. Hii hi hatari kwani huenda tukashuhudia mimba za mapema vijijini mwetu. Kaunti iwajibikie suala hilo kwa kutuletea walimu wa ECDE ili kuendeleza masomo kwenye vituo vyetu ambavyo hadi sasa vimefungwa,” akasema Bw Salale.

Bw Dokota Wakati alisema ni jambo la kusikitisha kwamba jamii ya Waboni haina elimu ya msingi wala chekechea.

Bw Wakati alisema watoto wengi wa jamii ya Waboni wamepitisha umri wa kujiunga na shule kutokana na kukosekana kwa shule zinazohudumu eneo hilo.

Anasema ni wanafunzi wachache pekee ndio ambao wamesafirishwa maeneo mengine kusoma.

Aliitaka serikali kuanzisha angalau kituo cha pamoja cha ECDE ili wanafunzi Waboni wapate elimu.

Naye Bi Amina Alale aliiomba serikali ya kitaifa kufikiria kuzifungua shule zote tano za msingi za Basuba.

“Usalama umeimarishwa eneo letu na sioni sababu ya shule zetu kuendelea kufungwa. Wakati umewadia kwa serikali kuu kuzifungua hizi shule na kutuletea walimu wa kutosha watakaohudumia watoto wetu,” akasema Bi Alale.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu Msimamizi wa Idara ya Elimu Kaunti ya Lamu, Bw Shee Sagara, alisema mipango inaendelea ili kuajiri walimu wa chekechea eneo la Basuba.

Alisema wamekuwa wakipata changamoto kila wanapotangaza nafasi za ajira eneo hilo.

Anasema wengi wa waliohitimu kufanya kazi hizo huwa hawako tayari kufanya kazi Basuba kwa kuhofia usalama wao.

Anasema kaunti aidha imejitahidi kusafirisha wanafunzi zaidi ya 280, wakiwemo wale wa shule za msingi na chekechea kutoka eneo la Waboni hadi Mokowe ili kusoma.

“Ni kweli. Shule za ECD eneo la Basuba zimefungwa. Tulikuwa tumeajiri walimu kwa kandarasi na punde kandarasi yao ilipoisha hatujaajiri wengine. Wengi hawataki kufanya kazi Basuba. Tayari tumeteua walimu watatu wa ECD ambao wanaendelea kupokea mafunzo vyuoni. Punde watakapohitimu tutawafikisha Basuba kufunza,” akasema Bw Sagara.