Lugha, Fasihi na Elimu

Mjadala Afrika: Kiswahili kina nafasi gani katika Umoja wa Afrika?

Na JOHN KOBIA December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WIKI iliyopita wanaowania nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) walishiriki katika mjadala ambapo walieleza sera, mipango na maono yao kuhusu mustakabali wa bara la Afrika.

Ingawa mjadala huo uliendeshwa kwa lugha za Kiingereza na Kifaransa, lililobainika ni kuwa Kiswahili kina mustakabali mwema.
Mjadala huo uliofanyika Ijumaa jijini Addis Ababa, Ethiopia, uliwashirikisha wagombea watatu: Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti, Raila Odinga wa Kenya na Richard Randriamandrato wa Madagascar.

Jambo la kwanza linalodhihirisha kwamba Kiswahili kina mustakabali mwema ni anwani ya mjadala huo: Mjadala Afrika. Kwa kuamua kutumia maneno ya Kiswahili ni ishara kwamba Kiswahili kinatambuliwa kama lugha ya kuunganisha watu wa bara la Afrika.
Umoja wa Afrika (AU) unatambua Kiswahili kama nyenzo muhimu ya mawasiliano.

Itakumbukwa kwamba mnamo 2022, Umoja wa Afrika uliidhinisha Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha rasmi za kuendesha shughuli zake. Hii ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya Kiswahili. Hatua hii itawezesha Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano mapana Afrika katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Umoja wa Afrika unatambua Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana ili kuuwezesha kuafikia malengo yake. Umoja wa Afrika umetafsiri baadhi ya stakabadhi zake kwa Kiswahili. Hii ni hatua ya kupongezwa katika juhudi za kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Afrika.

Katika Mjadala Afrika, wagombea walijadili namna ya kutekeleza ruwaza ya Afrika iitwayo: Ajenda 2063: Afrika Tuitakayo. Ajenda 2063 inalenga bara lenye maendeleo endelevu, umoja, amani na linaloendeshwa na watu wake. Ili kufikia malengo ya Ajenda 2063, ni muhimu bara la Afrika litumie lugha inayoweza kuwaunganisha watu wote wa Afrika. Kwa maoni yangu, lugha hiyo ni Kiswahili.