Wito wa mwandishi na msomi Wole Soyinka kuhusu Kiswahili kama lingua franca ya bara Afrika
JUMA lililopita, nilidai kwamba Kiswahili kimekwisha kupigiwa upatu kuwa lingua franca ya bara la Afrika. Kwa nini?
Baadhi ya wataalamu na watu maarufu waliowahi kuipigia kura lugha hii kuchukua nafasi hiyo ni pamoja na mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Nobel, Wole Soyinka (1986), Chinua Achebe (Naijeria), Ayi Kwei Armah (Ghana), Ngugi wa Thiong’o, Mohamed Hassan Abdulaziz, Ali Mazrui, Alamin Mazrui (Kenya), na Julius Malema (Afrika Kusini), miongoni mwa wengine.
Akiongea katika mkutano wa kwanza wa Festival of Arts and Culture (FESTAC) nchini Naijeria mnamo 1977, Soyinka alisema: “Ni masikitiko makubwa kwamba muungano huu (wa waandishi), umedumu kwa miaka ishirini tangu kufanyika kwa Kongamano la Pili la Waandishi wa Afrika huko Roma, Italia – ambapo ilipendekezwa kuteuliwa kwa mojawapo ya lugha za Kiafrika.
Tumeamua kwa kauli moja, baada ya kutafakari kwa kina, kwamba Kiswahili ndiyo lugha inayofaa zaidi kwa azma hii. Tunawarai waandishi wote kutekeleza mkakati huu; iwe ni mtu binafsi au kwa pamoja, katika kiwango cha bara, kukuza Kiswahili kwa maslahi ya bara Afrika sasa na siku za usoni.”
Soyinka aliongezea: “Kuhusiana na hili, tumependekeza kwamba Shirika la Uchapishaji la Afrika lililopendekezwa kuundwa litekeleze sera ya kutafsiri kila kazi inalochapisha kwa Kiswahili. Tunahimiza shule zote kuchapuza mchakato huu kwa kufundisha somo la Kiswahili badala ya masomo ya kigeni kama vile Ustaarabu wa Ufaransa, Historia ya Kijamii ya Waingereza, n.k.”