Kukuza na kutukuza Kiswahili ni kujitolea mhanga kwa hali na mali
BILA shaka wengi wetu tunajua kwamba wiki hii kulikuwa na kongamano la Kiswahili lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili Zanzibar kisiwani Pemba. Kongamano hilo lililofana sana lilikamilika siku ya Jumatano tarehe 18-12-2024.
Ndugu wapendwa nina imani thabiti kwamba mlipokuwa mkifuatilia na kuchungulia orodha ya majina mlishuhudia kwamba waliojisajili kushiriki kwenye kongamano hilo wengi walikuwa kina nani? Wa wapi na walitoka katika nchi zipi? Udadisi huo utakusaidia king’amua kwamba kuhudhuria makongamano si kazi rahisi mpaka kwanza uangalie umbali wa safari na uzito wa gharama.
Umbali pamoja na uzito huo wa gharama, huwalazimu wapenzi wa Kiswahili kuchukua uamuzi mgumu kwamba ama waende kushiriki kongamano au wasalie majumbani kwao katika nchi zao!
Ukweli ni kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kutenda lisilowezekana. Kila juhudi hutegemea uwezo wa mtu. Hapo ndipo nikagundua kuwa watu wengi wana ari ya kukiinua Kiswahili lakini ukuzaji na utukuzaji wa Kiswahili ni ghali mno! Ni gharama kubwa kiasi cha kutaka kujitoa mhanga na kujifunga kumbuu!
Kila mpenzi wa Kiswahili alitamani kusafiri afike Pemba kuhudhuria kongamano lakini bila kugugumiza wala kudodosa, ziara yenyewe iliwatanza watu wengine kutokana na umbali kutoka maeneo wanayoishi hadi Darisalama kufika Zanzibar kisha Zanzibar mpaka Pemba!
Hayo ni masafa yanayowezekana tu kwa kujifunga kibwebwe na kujitoa sadaka kwa hali na mali kutumikia Kiswahili!