Michezo

Asamba alenga makuu riadha za Dunia 2025

Na CECIL ODONGO December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MTIMKAJI wa mbio fupi Dan Kiviasi Asamba amesema analenga kungáa kwenye Riadha za Dunia za Ukumbini mnamo Machi na Riadha za Dunia mnamo Oktoba mwaka 2025.

Riadha za Dunia za Ukumbuni zitafanyika China mnamo Machi na ile ya Dunia itafanyika Septemba Tokyo Japan. Asamba ambaye hutimka mbio za mita 100 na mita 200, Jumanne alitajwa Mshindi wa Dhahabu wa Shindano la Tujiamini Initiative.

“Nimekuwa nikiimarika sana uwanjani na ushindi huu ni idhibati tosha kuwa juhudi ambazo nimekuwa nikiweka kwa muda wa miaka 10 hazijaenda bure,

“Sasa nina vifaa na mafunzo ya kisayansi ambayo yatanisaidia kujiandaa kwa mbio za mwaka ujao na nina imani nitatamba,” akasema Asamba akiwa mwenye furaha riboribo baada ya kushinda tuzo hiyo ya hadhi.

Mkimbiaji wa mbio fupi Dan Asamba akionyesha hundi ya Sh500, 000. PICHA|HISANI

Kwenye taaluma yake kama mkimbiaji wa mbio za masafa mafupi, Asamba amewakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ya hadhi. Alishindia Kenya dhahabu katika mbio za Afrika zilizofanyika kule Mauritius mnamo 2022.

Asamba ni askari wa gereza na mwanachama wa kikosi cha wanariadha kinachofamika kama Utawala Star Sprints Club.  Ushindi wake ulitamatisha misururu ya mashindano ya Tujiamini Initiative ambayo imekuwa ikiendelea tangu Februari 24.

Mashindano hayo yamefanyika katika maeneo manane huku ikitambua na kukuza vipaji vya wanaspoti mbalimbali. Washindi 750 walitunukiwa medali ya dhahabu, fedha na shaba kwa kungáa katika fani mbalimbali kwenye mashindano yenyewe.

“Asamba ni mtimkaji bora zaidi katika idara ya magereza na alistahili tuzo hii kutokana na kujituma kwake. Tuzo hii itamsukuma ajitume zaidi na kushinda nyingine anapolenga kufikia upeo wa taaluma yake,” akasema Kocha na mwanzilishi wa Utawala Sprints club Perpetual Mbutu.

Dan Asamba ajawa na furaha tele baada ya kutuzwa na SpotPesa. PICHA|HISANI

Mkuu wa mipango DBA Afrika Pius Shiundu alisema udhamini ambao wamekuwa wakitoa kwa wanamichezo umesaidia kutambua talanta mashinani.

“Tuzo hii si ya kumsherehekea tu bali inaashiria hatua kubwa aliyopiga kwenye taaluma yake. Akijituma zaidi, atafanikiwa kusherekea ufanisi mwingine zaidi,” akasema Shiundu.

DBA imekuwa ikishirikiana na Sportpesa kudhamini misururu ya  Tujiamini Initiative kote nchini.