• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
Monaco iliyokuwa ngome ya vipaji vya soka imesalia gofu tu

Monaco iliyokuwa ngome ya vipaji vya soka imesalia gofu tu

Na CHRIS ADUNGO

MWISHONI mwa wiki, kikosi cha AS Monaco kilimwajiri upya kocha Leonardo Jardim kwa mkataba wa miaka miwili na nusu baada ya kumtimua Thierry Henry katika tukio ambalo nahodha huyo wa zamani wa Arsenal amesema ni la kumvunja moyo, kusikitisha na kuhuzunisha sana.

Kutimuliwa kwa Henry ambaye hii ni mara yake ya kwanza katika ulingo wa ukocha kulitokana na matokeo duni ya Monaco ambao hadi kufikia sasa, wananing’inia padogo mkiani mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Katika sehemu ya taarifa ya kuteuliwa upya kwa Jardim, 44, Naibu Mwenyekiti wa Monaco Vadim Vasilyev alisema kufutwa kwa kocha huyo mnamo Oktoba ni hatua iliyofikiwa mapema sana na usimamizi bila makini.

“Jardim alifaa kupokezwa nafasi nyingine ya kuendelea kudhibiti mikoba ya kikosi. Ingawa Monaco ilipoteza wachezaji wengi katika mihula miwili iliyopita ya uhamisho, usimamizi ulikosea pakubwa katika harakati za kujaza baadhi ya mapengo,” akatanguliza.

“Hali hii haikutuwezesha kusuka tena kikosi imara chenye uwezo wa kukabiliana vilivyo na mawimbi ya ushindani. Maamuzi ya kumtimua Jardim hayakuwa bora,” akaongeza.

Japo Vasilyev alikiri kwamba Henry ni miongoni mwa wakufunzi wanaopenda sana kazi zao, majeraha ya mara kwa mara yaliyowakabili wachezaji wake ni miongoni mwa mambo yaliyomkosesha fursa ya kuwatambisha Monaco.

Chini ya Henry, Monaco walijipata katika ulazima wa kumsajili beki mzawa wa Brazil, Naldo kutoka Schalke, beki Fode Toure ambaye ni Mfaransa aliyetokea Lille na kiungo Cesc Fabregas aliyeagana na Chelsea mwezi huu. Hata hivyo, kichapo cha 5-1 ambacho Monaco walipokezwa na Strasbourg ligini katika mchuano wa mwisho chini ya Henry kiliwasaza katika hatari ya kushushwa ngazi.

Monaco ambao walitawazwa mabingwa wa Ligue Cup mnamo 2016-17 chini ya Jardim, walisajili ushindi mara tano pekee chini ya Henry katika mapambano yote.

Tangu watie kapuni ufalme wa Ligue 1, Monaco walipoteza huduma za Kylian Mbappe (PSG), Benjamin Mendy (Man City),Bernardo Silva (Man City), Tiemoue Bakayoko (Chelsea), Allan Saint-Maximin (Nice), Valere Germain (Marseille), Abdou Diallo (Mainz), Nabil Dirar (Fenerbahce), Corentin Jean (Toulouse) na Thomas Lemar (Atletico Madrid).

Kufurushwa kwa Henry kambini mwa Monaco kunajiri wakati ambapo wachezaji nyota wa kale wanapania kutawala vilivyo taaluma ya ukufunzi. Miongoni mwao ni Ryan Giggs, Zinedine Zidane, Patrick Vieira na Stevan Gerrard.

Giggs na Vieira wamehi kuvalia jezi za Man-United na Arsenal mtawalia. Wengine ni Zinedine Zidane, John Terry na nyota wa zamani wa Liverpool Steven Gerrard ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Rangers nchini Scotland.? Hadi kuajiriwa kwa Henry kwa mkataba wa miaka mitatu kambini mwa Monaco, fowadi huyo wa zamani alikuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji waliotinga mduara wa tatu-bora kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka jana.

Alkitarajiwa kusaidiana vilivyo na Patrick Kwame Ampadu na Joao Carlos Valado Tralhao ambao pia waliajiriwa na Monaco kutoka kwa timu za chipukizi kambini mwa Arsenal na Benfica mtawalia.

Akiwa mchezaji wa zamani wa Monaco, Henry aliwachochea waajiri wake hao kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo 1997. Nyota huyo ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Juventus, Barcelona na New York Red Bulls alihusishwa na uwezekano mkubwa wa kujiunga na Aston Villa.

Jardim ambaye ni mzawa wa Ureno aliaminiwa kudhibiti mikoba ya Monaco mnamo 2014 na kukiongoza kikosi hicho kunyanyua ubingwa wa Ligue 1 mnamo 2017. Taji hilo lililokuwa la kwanza kwa Monaco kutia kapuni tangu 2000 lilitosha kukomesha ukiritimba wa Paris Saint-Germain (PSG) katika soka ya Ufaransa.

You can share this post!

MATESO: Atwoli ataka ajira za Uarabuni zichunguzwe

Ramos akiri kuteswa na penzi la kale, sasa halali

adminleo