Afya na JamiiMakala

Utafiti: Sigara utotoni husababisha matatizo ya mapema ya moyo

Na PAULINE ONGAJI December 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UTAFITI mpya umefichua kwamba uvutaji sigara kuanzia utotoni unaongeza hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo mapema maishani.

Aidha, utafiti huo umeonyesha kwamba watoto wengi wanaoanza kuvuta tumbaku katika umri wa miaka 10 au katika umri wa kubalehe, huendelea kufanya hivyo hata baada ya kutimu miaka ya ishirini.

Watafiti walifuatilia watoto 1,931 waliozaliwa miaka ya tisini kuanzia walipokuwa na umri wa miaka 10 hadi walipofika miaka 24.

Mwanzoni mwa utafiti huo, ni asilimia 0.3 pekee ya watoto waliokuwa wakivuta sigara katika umri wa miaka 10, lakini idadi hii iliongezeka na kufikia asilimia 26 walipofika katikati ya miaka 20.

Takriban thuluthi tatu ya wale walioanza kuvuta sigara utotoni au katika umri wa kubalehe, waliendelea hadi mwanzoni mwa utu uzima.

Matumizi ya kila mara ya tumbaku kuanzia umri wa miaka 10 kuendelea hadi miaka 24, yalihusishwa na asilimia 52 ya visa vya uharibifu wa moyo mapema maishani, ambapo matatizo haya yalikuwa pamoja na moyo kuvimba, moyo kupunguza uwezo wa kujilegeza, na shinikizo la damu, kufikia miaka 24.

Baada ya kuhusisha hatari zingine kama vile shinikizo la damu, uzani mzito kupindukia, moyo kuvimba na ulegevu, vichochezi vya moja kwa moja vya tumbaku vinavyosababisha moyo kuvimba kati ya umri wa miaka 17 na 24 vilikuwa asilimia 30.

Tafiti za awali kwa watu wakomavu zimeonyesha kwamba uvutaji sigara kuanzia umri wa kubalehe, huongeza hatari ya maradhi ya moyo kufikia umri wa makamo.

Hata hivyo, hakuna utafiti wa awali ambao ulichanganua ishara za mapema za uvutaji tumbaku kuanzia utotoni, kwa moyo.

“Ni hatari sana kuanza kuvuta sigara katika umri huu mdogo, huku visa vya ongezeko la idadi ya vijana walio katika umri wa kubalehe wanaovuta sigara za kieletroniki. Bidhaa za sigara hizi huwa na viungo hatari kwa mapafu, na pia husababisha hitilafu kwenye mapigo ya moyo, hali ambayo yaweza kusababisha uharibifu wa kiungo hiki. Wanaotumia sigara za kieletroniki pia bila kujua wanajiweka hatarini,” asema Andrew Agbaje, profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha Eastern Finland.

“Utafiti huu unaonyesha kwamba mbali na kusababisha hatari ya kukumbwa na maradhi ya moyo baadaye maishani, uvutaji sigara katika umri wa kubalehe, unasababisha uharibifu wa kudumu kwenye misuli ya moyo,” alisema Emily Bucholz, Profesa msaidizi katika Kitivo cha udaktari cha Chuo Kikuu cha Colorado School of Medicine.

Utafiti huo, ambao ni ushirikiano kati ya chuo kikuu vya Bristol na Exeter, nchini Uingereza na Chuo Kikuu cha Eastern Finland, ulichapishwa kwenye jarida la the Journal of the American College of Cardiology (JACC).