WHO: Wananchi wa mataifa maskini walipa pesa nyingi hospitalini
NCHI zimetenga bajeti kidogo kwa afya huku wagonjwa wengi kutoka familia maskini wakipitia changamoto ya kulipia ada za hospitali, Shirika la Afya Duniani (WHO) limebaini.
Ripoti iliyochapishwa na WHO inasema nchi ziligharimika zaidi wakati wa Mlipuko wa Covid-19 lakini kufikia 2022, mambo yalibadilika.
Licha ya matumizi ya pesa katika afya kuongezeka, kiasi kilichotumika kwa mtu mmoja kilishuka katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea.
“Haya yalijiri wakati serikali ziligharimika sana hali ambayo inaonyesha kuwa mgao wa afya katika jumla ya matumizi ya serikali ulishuka,” ripoti inaonyesha.
Katika nchi zenye mapato ya juu, hata hivyo, matumizi ya fedha katika sekta ya afya yalikuwa karibu na viwango vya 2021. Lakini jumla ya matumizi ya serikali ilienda chini.
Vile vile, ripoti hiyo imebaini utegemezi wa misaada kutoka nje umeongezeka katika mataifa ya mapato ya chini na ya kadri.
Kadhalika, wananchi wengi wanajilipia ada za hospitali katika nchi 30 za mapato ya chini na ya kadri.
“Katika nchi 20 kati ya hizi, zaidi ya nusu ya wagonjwa wanajilipia ada za matibabu. Hali hii inachangia kuendeleza umaskini,” ikasema WHO.
Na katika nchi tajiri, asilimia 20 ya matumizi ya afya iligharamiwa na wagonjwa hasaa wenye mapato ya chini.
Ripoti ya WHO ilichapishwa katika siku ya kuadhimisha mfumo wa Afya kwa Wote mnamo Desemba 12, 2024.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema: “Siku ya Afya kwa Wote ni ukumbusho kwamba kila mtu anaweza kupata huduma za afya anazohitaji, bila matatizo ya kifedha.”
Nchini Kenya, bajeti ya afya ya makadirio ya Julai 2024 ilikatwa kwa Sh6 bilioni.
Kamati ya Afya katika Bunge la Kitaifa ilihusisha hatua hii na kuondolewa kwa Mswada wa Kifedha wa 2024/2025 baada ya kushinikizwa na maandamano yaliyoendeshwa na vijana wa kizazi cha Gen Z.
Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Uhasibu ilionyesha Sh766 milioni ziliibwa kupitia malipo kwa wafanyakazi hewa.
Hii inaonyesha kuwa sekta ya afya si kipaumbele na kama hali itaendelea hivi, WHO inasema, ufikiaji wa Afya kwa Wote itasalia kuwa ndoto.
Haya yanajiri huku serikali ikiendelea kutekeleza bima mpya ya Afya ya Jamii (SHIF) ambayo imekumbwa na pingamizi na changamoto.
Kulingana na uchunguzi wa hivi punde wa maendeleo ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) uliofanywa na Muungano wa Hospitali za Kibinafsi Mashinani na Mijini Nchini, Wakenya 7 kati ya 10 hawathamini SHA.
Mnamo Oktoba 2023, Rais William Ruto alitia saini Mswada wa Huduma za Afya za Msingi 2023 kuwa sheria.
Kiongozi wa taifa alilenga kuimarisha kinga ya maradhi na utambuzi wa mapema hasaa katika vipindi vya milipuko.