• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Siogopi kutemwa ODM, nitachaguliwa tena nikipoteza kiti – Dori

Siogopi kutemwa ODM, nitachaguliwa tena nikipoteza kiti – Dori

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Msambweni Suleiman Dori Jumamosi alisema haogopi kufurushwa kutoka ODM akielezea imani kuwa atachaguliwa tena ikiwa atapoteza kiti chake na uchaguzi mdogo uitishwe.

Mbunge huyo ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa Kundi la Wabunge wa Pwani (CPG) alikariri kuwa katu hajuti kuunga mkono azma ya Naibu Rais kuingia Ikulu 2022.

“Ni haki yangu na kidemokrasia na kikatiba kuunga mkono kiongozi ninayempenda katika kinyang’anyiro kijacho cha urais 2022. Ikiwa ninafukuzwa ODM kwa sababu ya kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto basi sijuti kwani nitaendelea kumpigia debe,” akasema katika eneobunge lake.

Bw Dori ambaye anahudumu kipindi cha pili bungeni alisema hayo alipoongoza hafla ya kuchanga pesa za kusaidia kundi la akina mama la Kinondo, katika eneo la Nyumba Mbovu, eneobunge lake.

Mnamo Alhamisi Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la ODM liliidhinisha ripoti ya kamati ya nidhamu ya chama hicho iliyopendekeza kuwa Bw Dori na mwenzake wa Malindi Aisha Jumwa wafukuzwe chamani kwa kuunga mkono sera za mgombeaji urais wa chama kingine yaani Dkt Ruto wa Jubilee.

NEC pia ilipendekeza kuwa wawili hao waondolewe kama wanachama wa kamati za bunge walizoteuliwa kwa misingi ya kuwa si wanachama wa ODM.

Hii ina maana kuwa kiranja wa wachache bungeni Junet Mohamed sasa atakuwa huru kumwandikia Spika Justin Muturi akimtaka kuwaondoa wawili hao kutoka kamati husika.

Bi Jumwa huenda akapoteza nafasi yake katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC) yenye hadhi na marupurupu mengi. Vile vile atapokonywa nafasi yake katika kamati ya bunge kuhusu Huduma za Kijamii.

Naye Bw Dori atapoteza nafasi yake katika Kamati ya Uchukuzi na Nyumba inayoongozwa na Mbunge wa Pokot Magharibi David Pkosing.

Hata hivyo, kwanza uamuzi wa NEC sharti uidhinishwe na Baraza la Kitaifa la Utawala (NGC) la ODM ambalo huongozwa na kiongozi wa chama hicho Raila Odinga.

Baraza hilo linatarajiwa kukutana mwezi ujao wa Februari kuamua hatima ya Bw Dori na Bi Jumwa. Wanachama wa NGC wanajumuisha wenyeviti wa mataifa ya ODM katika kuanti zote nchini, wabunge, madiwani, maseneta na magavana waliochaguliwa kwa tiketi ya chama hicho cha chungwa.

Jumamosi Bw Dori alisema: “Uongozi hutoka kwa Mungu na ni yeye pekee ambaye ataamua ikiwa nitachaguliwa tena ama la. Ni watu wangapi walikuwa kwa ODM katika uchaguzi mkuu uliopita lakini wakapoteza?”

Mbunge huyo alisema atakubaliana na uamuzi wowote ambao utafanywa na baraza la NGC.

Bw Ali Mwangauri, ambaye ni mfuasi sugu wa Dori alisema atasimama mbunge huyo “kufa kupona”.

“Tuko na Mheshimiwa Dori hadi kifo kitakapotutenganisha!” akasema, akiongeza kuwa ataguru ODM ikiwa hakitabatilisha uamuzi wa kumtema mbunge huyo.

Lakini wafuasi wa Bw Omar Boga ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Dori katika uchaguzi mkuu wa 2017 waliitaka NGC iidhinisha uamuzi wa NEC haraka ili uchaguzi mdogo uitishwe.

You can share this post!

TAHARIRI: Tumuunge mkono Rais kuhusu ufisadi

Guikan agura Gor, ayoyomea Zambia

adminleo