Makala

Jinsi ya kujilinda dhidi ya walaghai wa mitandao msimu huu wa Krismasi

Na   WINNIE ONYANDO December 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HUU ni msimu wa kupumzika, kuburudika na kusherehekea.

Hata hivyo, ni kipindi ambacho wahalifu wanalenga Wakenya wanaofanya ununuzi mtandaoni na wanaotumia simu au kadi kulipia bidhaa walizonunua.

Utafiti uliofanywa hivi majuzi na Shirika la Kiteknolojia ya ControlD ulionyesha kuwa visa vya ulaghai mitandaoni viliongezeka mara dufu, huku baadhi ya wahalifu wakiwaibia watu pesa kwa kutumia maneno ya uongo na yanayovutia hisia zao.

“Kila mara tunashuhudia shughuli za ulaghai zilizoimarishwa wakati wa msimu wa Krismasi. Mara nyingi wahalifu hao hutumia arafa au mfumo wa malipo ya kielektroniki kama vile malipo kutumia M-pesa. Mwaka huu, visa vya uhalifu mitandaoni viliongezeka kwa asilimia kubwa,” akasema Yegor Sak, mtaalamu mwanzilishi wa ControlID.

Kwa upande mwingine, data iliyochapishwa na SlashNext’s, inaonyesha kuwa visa vya ulaghai viliongezeka kwa asilimia 703, mwaka huu, 2024.

Hii inaonyesha kwamba walaghai wanafahamu mbinu za kutumia ili kuwaibia watu.

Wahalifu hao wana uwezo kuunda tovuti ghushi na taarifa zisizo za kweli kama njia ya kulaghai watu na kuwaibia.

Baada ya kuvutia wateja, wao hutoa fomu ndefu za usajili ambazo zinahitaji watumiaji kujaza taarifa zao za kibinafsi na wakati mwingine, maelezo ya kadi ya benki.

Kuna wale wanaowapigia watu simu na kuwateka makini na baadaye kuomba taarifa za kibinafsi ambazo wanatumia kuiba pesa kutoka kwenye akaunti zao za M-pesa.

Mara nyingi huwa wanawataka watu kuwatumia marafiki zao jumbe hizo huku wakilaghaiwa kuwa wataongezwa pesa zaidi wakisambaza taarifa hizo kwa wenzao.

“Walaghai wanaweza pia kuunda kurasa bandia za kuingia. Ikiwa watumiaji wanajaribu kuingia kwenye akaunti yao, walaghai hupata taarifa zao na nenosiri zao (pin), na kutoa ufikiaji sio tu kwa akaunti za waathiriwa, lakini kwa habari zote za kifedha zilizohifadhiwa hapo. Kwa hivyo, ili kulinda data na fedha zako koma kutoa maelezo ya taarifa zako za kibinafsi kwa watu usiowafahamu. Ikiwa huna nambari za huyo mtu, usidhubutu kumpa nambari yako ya kitambulisho wala jina lako. Jilinde na marafiki zako wakati huu wa Krismasi,” akaongeza Bw Sak.

Ili kujilinda, unafaa kuchukua hatua zifuatazo:

Hakikisha unanunua kupitia tovuti salama

Kabla ya kununua bidhaa yoyote mtandaoni, hakikisha kuwa tovuti unayotumia ni halali na salama. Angalia ikiwa inaanza na https:// badala ya http://.

Pia, hakikisha kuna alama ya kufuli karibu na anwani ya tovuti, ambayo inaashiria kuwa mawasiliano yako na tovuti yanalindwa.

Tumia nenosiri ya kipekee

Nywila (nenosiri) dhaifu ni rahisi kugunduliwa na wadukuzi. Hakikisha unatumia nywila ya kipekee. Pia, epuka kutumia nywila moja kwa akaunti nyingi. Badala yake, tumia nywila tofauti kwa kila akaunti.

Kagua tathmini na maoni ya wateja

Kabla ya kununua kutoka kwa tovuti mpya, soma maoni na tathmini za wateja wengine.

Tovuti nyingi bandia zinaonyesha bidhaa nzuri kwa bei za chini, lakini wateja wanapolipa, wanatumiwa bidhaa ghushi au hata kupoteza pesa zao.

Tumia njia salama za malipo

Daima tumia njia salama za malipo, kama vile kadi za mkopo au mifumo ya malipo ya kidigitali kama PayPal, ambazo zinatoa ulinzi wa ziada dhidi ya ulaghai.

Epuka kutuma pesa taslim kwa akaunti za kibinafsi au kupitia njia ambazo haziwezi kufuatiliwa.

Weka programu za ulinzi

Kompyuta na simu za mkononi zinapaswa kuwa na programu za kupambana na virusi na zisasishe mara kwa mara.

Programu hizi zinaweza kusaidia kutambua na kuzuia programu hatari ambazo wahalifu hutumia kuiba taarifa zako binafsi.

Jitahadhari na ofa zinazovutia kupita kiasi

Iwapo ofa inaonekana kuwa nzuri kupita kiasi, kuna uwezekano mkubwa kuwa ni uhalifu.

Walaghai hutumia ofa za uongo kuvutia wateja na kuwaingiza katika mitego yao kisha kuwaibia.

Kumbuka kuwa uhalifu mitandaoni unaweza kuharibu furaha ya Krismasi ikiwa hutakuwa mwangalifu.

Kwa kufuata hatua hizi za kujilinda, unaweza kufurahia msimu huu wa sikukuu bila wasiwasi wa kupoteza pesa au taarifa zako binafsi.