Serikali kuzindua lebo ya kidijitali kutambua mifugo Kenya
SERIKALI inapanga kuzindua lebo ya kidijitali kutambua idadi ya mifugo Kenya, na jinsi inavyofugwa.
Katibu katika Idara ya Ustawishaji na Maendeleo ya Mifugo, chini ya Wizara ya Kilimo, Jonathan Mueke amesema lebo hiyo itakuwa na GPS – mfumo wa urambazaji unaotegemea setilaiti, na ambao hutoa taarifa za eneo, kasi, na muda mahali popote duniani.
Bw Mueke, kwenye kikao na wanahabari Jijini Nairobi, alisema mpango huo umekuwa ukijaribiwa kwa zaidi ya miaka 20 bila mafanikio, na serikali ya sasa imepata ufanisi.
“Mtandao huo unaojulikana kama Anitrack (Animal tracker) utasaidia kusajili mifugo, kuwatambua, kujua bridi, kiwango cha mazao yao na maeneo ya nchi wanayotoka,” Katibu Mueke alisema.
Kwa muda mrefu Kenya imekuwa ikikosa kuwahi masoko yenye ushindani mkuu ng’ambo ya bidhaa za mifugo, na hatua hiyo serikali inaamini itasaidia kuziba gapu hiyo.
Lebo ya kidijitali kwa mifugo, Bw Mueke alihoji itafanikisha kuboresha usalama wa bidhaa za mifugo; nyama, maziwa, mayai na ngozi.
“Masoko ya ng’ambo yanataka kujua mazao ya kilimo; ya mimea na mifugo yanakotoka. Mpango huo wa 2025 utatusaidia kujua wakulima na wafugaji wetu,” alielezea afisa huyo.
Anitrack, Bw Mueke alisema itasaidia pakubwa kukabiliana na kero ya wizi wa mifugo hususan maeneo kame.
Kwa muda mrefu, kaunti zilizoko maeneo kame zimekuwa zikishuhudia uhalifu kufuatia wizi wa mifugo.
Baadhi ya familia zimehama makwao kwa hofu ya kuvamiwa na majangili wanaolenga kuiba mifugo, wengine jamaa zao wakiuawa.
Kaunti tajika kwa wizi wa mifugo zinajumuisha Elgeyo – Marakwet, Baringo, Samburu, West Pokot, Laikipia, Samburu na Turkana, Katibu Mueke akisema mfumo huo wa kidijitali utasaidia serikali kujua iliko mifugo inapoibwa.
“Lebo ya GPS itatufaa sana kufuatilia mifugo inapoibwa.”
Afisa huyo, hata hivyo, hakuelezea iwapo lebo hiyo itakuwa fiche ili kukwepa kutolewa na wahuni.
Isitoshe, hakufichua bajeti iliyotengewa mpango huo.
Kando na kukabiliana na kero ya wizi na kuhakikisha bidhaa za mifugo zinakuwa salama kwa minajili ya masoko ng’ambo, alisema utambulisho huo wa wanyama wa nyumbani utakuwa afueni kwa wakulima kwani utatumika kuchukua mikopo benkini.
Kwa sasa, mashirika ya kifedha hayawapi wafugaji mikopo kwa kutumia mifugo kwa hofu ya kukosa mbinu kuwasaka wanapokataa kurejesha fedha.
Huku mpango huo ukiashiria kupokea pingamizi, Bw Mueke amevitaka vyombo vya habari kuwa makini dhidi ya habari potovu zinazoendeshwa mitandaoni.
Amefutilia mbali tetesi kuwa teknolojia ya kutambua mifugo inalenga kuanza kutoza ushuru wakulima.
“Mitandaoni, tumeona baadhi ya watumiaji wakidai mpango wa kuandikisha mifugo kupitia mfumo wa kidijitali ni njia ya kutaka kutoza ushuru wafugaji kama vile wa kuku, sungura na wengineo. Huo ni uongo mtupu,” akasema.
Alisisitiza lengo la mpango huo ni kuboresha usalama wa bidhaa za mifugo.