Uncategorized

Wapenzi wa Kiswahili waomboleza kifo cha msomi na msimamizi wa idara Chu Kikuu cha Moi

Na TITUS OMINDE December 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WASOMI wa Kiswahili wanaendelea kuomboleza kifo cha msomi na mwenyekiti wa idara ya Kiswahili na Lugha nyingine za Kiafrika chuoni Moi, Dkt Allan Opijah.

Msomi huyo ambaye alijikita sana katika kazi za utafiti kwenye Lugha ya Kiswahili, alifariki akiwa na umri wa miaka 70.

Alifariki asubuhi ya Desemba 21, 2024 nyumbani kwake mtaani Kapsoya mjini Eldoret baada kuzirai kutokana na kufeli kwa moyo maarufu heart failure.

Marehemu amekuwa akiugua maradhi ambayo yanafungamana na moyo, miongoni mwa matatizo mengine ya kiafya kabla ya kifo chake.

Dkt Opijah anatambuliwa na wengi hasa wanafunzi wake ambao walipata nafasi ya kutagusana naye katika Chuo kikuu cha Moi kama mwalimu na mshauri mnyenyekevu.

Msomi na mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili na Lugha nyingine za Kiafrika Chuo Kikuu cha Moi, Dkt Allan Opijah, akihutubu hapo awali. PICHA|CHRIS ADUNGO

Alitarajiwa kupandishwa hadhi hadi kuwa profesa mwaka ujao, 2025.

Kabla ya kifo chake, alikuwa amezama na kuibuka na machapisho mbalimblai yakiwemo, Mitindo ya Lugha Ibuka katika Mitandao ya Kijamii: Mifano kutoka Mawasiliano ya Facebook, Mulika Journal (2018), Uchanganuzi wa makosa ya Kiisimu katika matumizi ya Kiswahili miongoni mwa Wanyore (2004) A Tool for Development: The Multidisciplinary Approach, Moi University Press (2001).

Uswahilishaji wa istilahi katika baadhi ya vipengele vya taaluma ya Uchanganuzi Usemaji: Mfuatano, Udokezwa na Matendo Usemi (2000) pia zilikuwa kazi zake nyingine alipotafiti kuhusu Kiswahili.

Katika wingi wa chapisho zake, alishikirikiana na marehemu Profesa Naomi Shitemi miongoni mwa wengine.