Habari za Kitaifa

Hatimaye Martha Karua apata leseni ya kuwakilisha Besigye kortini Uganda

Na  SAM KIPLAGAT January 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKILI wa Kenya Martha Karua, ambaye ni kiongozi wa chama cha Narc Kenya, amepewa leseni maalum kumwakilisha kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye katika kesi inayoanza leo baada ya kuwasilisha tena ombi lake

Baraza la Sheria la Uganda, ambalo hutoa leseni kwa mawakili kufanya kazi nchini humo, mwaka jana lilikataa ombi la Bi Karua, Dkt Besigye na Hajji Obeid Lutale walipowasilishwa mbele ya mahakama ya kijeshi.

Bi Karua aliwasilisha ombi lake tena Desemba 23, na wanachama wa baraza hilo kwa uamuzi wa pamoja, wakakubali kumpa leseni hiyo.Karua ataongoza mawakili kadha wa Dkt Besigye na Bw Lutaale.

Likikataa ombi hilo Desemba 6, baraza hilo lilidai kuwa nia ya Bi Karua haikuwa ya kitaalamu.”Imeonekana kutokana na maombi kwamba nia yako si ya kitaalamu tu, inachochewa na ajenda ya kisiasa,'”Bi Margaret Navakooza alisema katika barua.

Barua hiyo iliongeza kuwa ombi hilo halikuwasilishwa kwa mujibu wa Sheria ya sasa ya Mawakili na kuwa halikuambatishwa na nakala za vyeti vya Bi Karua kutoka kwa Chama cha Wanasheria wa Kenya miongoni mwa stakabadhi nyingine.

Hatua ya kukataa ombi la Bi Karua ilisababisha chama cha wanasheria katika Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Uganda mbele ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.

Chama cha wanasheria wa kikanda kilisema kunyima Bi Karua leseni maalum ya kuhudumu Uganda hakuendani na wajibu wa kukuza upatanishi wa taaluma ya sheria chini ya Kifungu cha 126 cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

EALS ilisema kuwa mawakili wamekuwa wakikabiliwa na matatizo katika harakati zao za kuvuka mipaka kufanya kazi na kulaumu nchi washirika kwa kushindwa kuhitimisha makubaliano kuhusu huduma za kisheria.

“Kwa hivyo unatakiwa kuwasilisha jibu ndani ya siku 45 kuanzia siku ya kukabidhiwa barua hii. Ukikosa kufanya hivyo, kesi itasikilizwa na kuamuliwa bila wewe kuwepo,” ilisema notisi ya Msajili wa mahakama kwa Mwanasheria Mkuu wa Uganda.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA