MAONI: Inawezekana Natembeya anatembea na wananchi
KATIKA mazishi ya mamake spika wa bunge Moses Wetang’ula, siasa za utekaji nyara zilisheheni.
Kuna baadhi ya viongozi waliosema kuwa vijana wanaodaiwa kutekwa nyara na maafisa wa polisi ama watu wanaodhaniwa kuwa polisi ni waongo.
Eti wanajiteka wenyewe ila baadhi wamepatikana wamefariki. Mmoja wa wanasiasa waliozua gumzo kubwa kwa hilo ni George Natembeya, gavana wa Trans – Nzoia.
Chini ya dakika mbili Natembeya alikuwa amewasha mtandao kwa hoja zake alizoratibu kwa mantiki kubwa.
Kwanza alianza kuzomewa alipopewa kipaaza sauti na watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa spika wa bunge Moses Wetang’ula.
Kwa haraka, dadake Wetang’ula aliingilia kati na kuwaonya wasiharibu maombolezi ya mamake.
Natembeya alipoanza yake alisema mambo hatari kwa wenyeji wake na kuu zaidi kwa Rais ambaye alikuwa miongoni mwa waombolezaji.
Alitanguliza kuwakumbusha waliompigia kelele kuwa watumie midomo yao kwa kazi ya maana.
Na akawajuza waombolezaji kuwa kifo kinaweza kumpata yeyote na ana marafiki katika boma hilo akiwemo Tim Wanyonyi kakake Wetang’ula ambaye ni mbunge wa Westlands.
Ujasiri wake ukazidi kuongezeka. Akasema kuwa anashangaa watu wana vyeo vikubwa serikalini lakini wanasubiri fursa za mazishi ili kuomba misaada na mafao mengine kwa Rais.
Kama hilo halikutosha akaingia katika suala walilotaka kulisikia wengi: utekaji nyara wa vijana.
Akakanusha ya viongozi waliomtangulia kwa hoja.
Akamkumbusha rais kuwa utekaji nyara wa vijana ni tabia mbovu inayostahili kukomeshwa kwa dharura. Watu walibaki midomo wazi.
Mfalme alikuwa amepata ujumbe kutoka kwa ‘mtu mdogo’. Watu wakashangilia.
Kumjibu Natembeya kulihitaji hekima kiasi fulani wala si jazba za kiongozi wa walio wengi bungeni Kimani Ichung’wa. Alifanya wanavyosema vijana wa leo kuwa “kuchoma”.
Ichung’wa kwa maoni yangu alivuka mipaka na kutoka nje ya mada na kufanya shambulizi binafasi kwa Natembeya ambaye alikuwa akipiga tabasamu alikokuwa kaketi.
Alibwaga bila mpangilio hoja za msitu wa Mau ambazo hazikuwa zikiendana na hadhira lengwa. Alikuwa kajiingiza kwa mtego wa Natembeya kwa kujua ama kutofahamu. Hilo lilikuwa dogo.
Kuu zaidi ni kuwa Natembeya alimfanya Rais kuzungumzia suala hilo kwa hiari ama shuruti. Rais Ruto alisema kuwa serikali haihusiki kamwe na utekaji nyara.
Akaitaka idara ya polisi kufanya kazi yake. Hili ukilitazama kwa jicho la ndani linaonesha kuwa hoja ya Natembeya aliisuka kwa namna ya kumgusa Rais hata akalizungumzia suala hilo.
Na Rais wetu ambaye hupendelea kubuni na kupanga ahadi nyingi alikuwa mchache wa hulka hiyo pendwa kwake. Hakuyajibu matakwa ya viongozi waliozungumza kabla yake na kuwahakikishia Wakenya yalivyo mazoea yake.
Natembeya amefanywa mjadala wa taifa. Inawezekana ana nyota ya kutembea na watu.
Paul Nabiswa ni Mhariri, NTV