Kipigo cha Arsenal mikononi mwa Newcastle chaambia Arteta anahitaji straika
LONDON, Uingereza
ARSENAL wako mguu mmoja nje ya fainali ya kipute cha League Cup almaarufu Carabao, baada ya kukosa kutumia nafasi zao vyema wakiaibishwa 2-0 na Newcastle katika nusu-fainali ugani Emirates, Jumanne.
Wanabunduki hao, ambao mara ya mwisho walitawala League Cup ni msimu 1992-1993, walipata pigo katika juhudi za kumaliza ukame huo baada ya kuzamishwa na mabao kutoka kwa Alexander Isak na Anthony Gordon.
Arsenal walikuwa juu karibu katika kila idara ikiwemo makombora 23-7, umilikaji mkubwa wa mpira (asilimia 70), pasi 571 dhidi ya 258 na kona 11-1, lakini hawakutumia nafasi zao kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza.
Gabriel Martineli na Kai Havertz walipata nafasi mbili za wazi.
Shuti la Martinelli lilipiga mwamba nacho kichwa cha Havertz kikajaa nje.
Ni mchuano unaoweka wazi kuwa kocha Mikel Arteta anafaa kusaini mshambulizi wakati wa kipindi kifupi cha uhamisho cha mwezi huu wa Januari.
“Ukitazama kile timu zote zilionyesha uwanjani, matokeo haya hayaonyeshi picha kamili ya mechi. Hata hivyo, ukweli ni kuwa wapinzani wetu walikuwa wazuri sana katika kutumia nafasi zao nasi tuliziuza,” akalia Arteta.
Mhispania huyo alilaumu mpira wa Puma unaotumiwa katika Carabao akisema ni tofauti na ule wa Nike unaotumiwa kwenye Ligi Kuu. “Tulipiga mipira mingi juu ya mwamba na inasikitisha kuwa mpira huu unapaa sana,” akasema Arteta.
Ni mara ya kwanza Newcastle ilipata ushindi bila ya kuwa na Bruno Guimaraes. Katika mechi saba Mbrazil huyo amekosa tangu ajiunge na Newcastle mnamo Januari 2022 kutoka Lyon, Magpies hawakuwa na ushindi. Guimaraes pamoja na mchezaji mwenza Fabian Schar walikuwa mashabiki dhidi ya Arsenal wakitumikia adhabu.
“Tulishinda leo bila wachezaji hao wawili ambayo ni ishara nzuri sana kwetu kwa sababu inayonyesha tuna nguvu na pia wachezaji wanaoweza kujaza nafasi zao,” akasema kocha wa Newcastle, Eddie Howe.
Mechi ya marudiano ni Februari 5 wakati Arsenal watazuru ugani St James’ Park. Nusu-fainali ya pili kati ya Tottenham na Liverpool iliratibiwa kusakatwa Jumatano usiku.
Liverpool ni mabingwa watetezi na pia washikilia wa rekodi ya mataji mengi ya Carabao (10).