Maoni

MAONI: Hivi dunia ikiongozwa na Putin, jasusi na mshindani mkuu wa Amerika, itakuwaje?

Na DOUGLAS MUTUA January 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

NADHANI sitakuwa nimekosea nikisema kuwa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaliongozwa na roho wa Mungu yalipokataa ombi la Sudan kujiunga na Jumuiya hiyo.

Ama kweli, mataifa ya kuvuliwa kofia kwa kupinga ombi hilo ni Tanzania na Uganda kwa kuwa mengineyo – Kenya, Burundi na Rwanda – yaliunga mkono ombi hilo la mwaka 2011.

Uamuzi huo wa busara usingefanywa, mauaji ya halaiki yanayoendelea Sudan yangekuwa na athari mbaya zaidi kwa eneo hili, sikwambii na mibabe wa siasa za kimataifa kama vile Amerika na Urusi wangekuwa wanatutumuliana misuli kwenye ardhi yetu.

Wakimbizi wangekuwa wametapakaa kote Afrika Mashariki kwa kuwa mataifa wanachama yalikwisha kuondoa hitaji la viza ya kusafiria kwa wananchi wao.

Hata wewe kwenu kukiwa na vita utakimbilia eneo salama, hasa ambalo huitishwi viza ukivuka mpaka.

Wala tatizo la wakimbizi halingetupa hofu kuu mno – hasa kwa kuwa mkimbizi ni mtu wa kuonewa imani badala ya kufukuzwa – likilinganishwa na lile la mataifa hayo makuu duniani kutumia ardhi yetu kama jukwaa la kuendeshea vita vyao.

Hilo la mwisho lingekuwa hatari mno kwa kuwa, japo hivi majuzi Amerika imeilaumu Urusi kwa kufadhili pande zote mbili zinazopigana, lawama hizo zinatarajiwa kutosikika tena tarehe 20 mwezi huu, siku tisa pekee zijazo.

Kisa na maana? Bw Donald Trump ataapishwa kuwa rais wa Amerika, na si siri kwamba anamuenzi na kumsujudia Rais Vladmir Putin wa Urusi. Atawezaje kumkanya au kumkomesha mtu anayemchukulia kuwa shujaa wake?

Angekuwa anaapishwa mtu mwingine yeyote kuwa rais wa taifa hilo tajiri na lenye nguvu zaidi duniani, ningekwambia usiwe na hofu yoyote kwa kuwa atadhibiti hali. Linalotabirika wakati huu ni kwamba Trump atavuruga mambo!

Trump ni mtu tofauti sana asiyeheshimu wala kutambua sera za Amerika za mahusiano ya kimataifa, hivyo uhusianio wake na Putin utakuwa na athari kubwa katika vita hivyo. Ole wao maskini raia wa Sudan wanaoteswa na kuuawa kila siku huku!

Amini usiamini, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba Trump atamwacha Putin kujifanyia atakayotaka, labda hata atamhimiza kuyafanya. Ataupa kipaumbele urafiki wao na kusahau hata vikwazo ambavyo juzi Amerika imemwekea mmoja wa viongozi wa vita hivyo.

Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ama ukipenda Hemedti kwa jina la msimbo, anayeongoza majeshi maalum yanayopigana na jeshi la taifa la Sudan, amewekewa vikwazo kwa madai kuwa wapiganaji wake wanaua kwa nia ya kuyaangamiza makabila fulani.

Wapiganaji hao pia wamelaumiwa kwa kuwabaka wanawake na kuwazuia raia wanaojaribu kutafuta misaada ya chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu kufika iliko, hivyo kusababisha vifo vyao.

Huenda lawama kama hizo hutazisikia tena Trump akichukua usukani wa serikali ya Amerika kwa kuwa, ikiwa kwa hakika Urusi inafadhili vita hivyo, hatataka kumkasirisha Putin.

Kumbuka Putin hajaficha furaha yake kwamba Trump anarejea Ikulu ya White House, alimoondoka miaka minne iliyopita. Haikosi anaangua kicheko akitafakari kuhusu mambo yatakavyomwendea vyema katika muda wa miaka minne ijayo.

Putin ametamani sana kuishi katika dunia ambapo hazuiwi na yeyote kufanya chochote, hakuna anayemtishia, na kila mtu duniani anajua kwamba ndiye mshawishi mkuu wa mahusiano ya kimataifa.

Anajua rafiki yake – Trump, ambaye ameapa kuyamakinikia zaidi masuala ya ndani kwa ndani yanayowahusu Waamerika badala ya kujaribu kuwa polisi wa dunia – atamwachia uwanja huo wa siasa za kimataifa acheze mpaka achoke.

Tafakari kuhusu dunia ikiongozwa na Putin, jasusi wa zamani ambaye ametafuta fursa ya kuishinda Amerika katika uga huo tangu alipoingia mamlakani takriban miaka 25 iliyopita.

Sudan ingekuwa mwanachana wa EAC, ungetarajia Putin ajaribu kueneza ushawishi wake katika eneo hili, adhibiti bandari zetu kuanzia Mombasa mpaka Kinshasa, mamluki wake ambao wameteka serikali nyingi za Afrika Magharibi wafanye mambo yao huku kwa raha zao.

Viongozi wa EAC wanapaswa kukaa macho kabisa, washikilie msimamo wa kutofungana na upande wowote katika misukosuko ya kimataifa, wawe watazamaji tu katika kipindi hiki cha mpito.

[email protected]