• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 1:25 PM
CHOCHEO: Mpikie mkeo akupe raha zaidi chumbani

CHOCHEO: Mpikie mkeo akupe raha zaidi chumbani

NA BENSONN MATHEKA

Wanaume wanaopikia wake zao na kusaidia majukumu ya nyumbani kama kulea watoto huwa na maisha ya ndoa yenye furaha. Watafiti wanasema siri ya kudumisha uhusiano wa kimapenzi wenye furaha kwa miaka mingi sio kuwa na mali nyingi, ni kusaidiana kwa majukumu na kushauriana kwa kila jambo.

Kulingana na tafiti mbalimbali, wanawake wanaotumia lugha ya heshima kuwaomba waume wao kusaidia kazi nyumbani hawajuti.

“Inaanza na lugha ambayo mtu hutumia kumuomba mchumba wake kitu au afanye jambo. Wanawake wanaotumia lugha ya heshima kuwataka waume zao kutekeleza majukumu ya nyumbani huwa ni furaha,” asema Mwanasaikolojia Jean Seager kwenye makala yaliyochapishwa mtandaoni.

Kulingana na Seager, wanawake huchukulia wale wanaosaidiwa majukumu ya nyumbani na waume wao kama wenye bahati.

“Sio kwamba huwa ni wenye bahati, huwa wamefanya kinachopaswa kwa kudumisha mawasiliano, kuheshimu na hata kuwafunza waume wao baadhi ya majukumu ya nyumbani. Ni makosa kwa wanawake kuamini kuwa wanaume wanaelewa majukumu yote ya nyumbani,” asema Seager.

Lakini anaonya kuwa inategemea mazingira ambayo mwanamume hutekeleza majukumu ya nyumbani ambayo kwa miaka mingi tamaduni nyingi zimeamini ni ya wanawake.

“Ukimkaripia mumeo ukimtaka apike ikiwa umetangulia kufika nyumbani na kuketi sebuleni kutazama runinga, utakuwa ukialika balaa. Ikiwa unashughulikia mtoto kisha umuombe asaidie kufua nguo, basi utakuwa umeshinda,” asema.

Wataalamu wa masuala ya ndoa wanasema kwamba kujitolea kwa wanaume kusaidia majukumu nyumbani kunaimarisha uhusiano, kuongeza mapenzi na kufanya ndoa kuwa yenye furaha.

“Kile ambacho wanatarajia ni heshima na ushirikiano kutoka kwa wake zao. Wanaume hawataki kukosolewa, wanataka kurekebishwa kwa lugha ya heshima,” asema David Okwemba wa shirika la Families for Tomorrow.

Kulingana na mtaalamu huyu, kila mwanandoa akitambua majukumu yake na kupalilia moyo wa kusaidiana, ndoa huwa haina budi kushamiri.

“Hapa ninamaanisha uwazi katika ndoa. Mwanamke hafai kuchelewa akipiga soga na wenzake na atarajie mumewe atayarishe chakula cha jioni. Akichelewa katika shughuli ya kufaidi familia, basi itakuwa vyema mumewe kumsaidia kupika,” asema.

Wataalamu wanasema japo ni muhimu kwa wanandoa kusaidiana, ni makosa kuiga mtindo wa wanandoa wengine. “Nimewasikia watu wakiwafananisha wanaume au wake zao na wengine. Hiyo haifai kwa sababu kila ndoa ni tofauti. Usimtake mumeo au mke kuwa kama wa rafiki yako, mazingira ya ndoa na hulka za watu huwa tofauti. Palilia uhusiano wako na mtu wako kivyako. Weka msingi wako kivyako ma ikishindikana, tafuta ushauri wa wataalamu,” asema.

Kulingana na utafiti wa chuo kikuu cha Chicago, Amerika, ndoa za watu wanaoiga marafiki wao hugeuka kuwa balaa ilhali za watu wanaotafuta ushauri kutoka kwa marafiki na familia huyumba baada ya muda.

“Ni ndoa za watu wanaosaidiana kwa uwazi, heshima na kushauriana wao wenyewe au na wataalamu zinazokuwa na furaha na kwa muda mrefu,” unasema utafiti huo.

Kulingana na tovuti ya www.luvze.com kusaidiana majukumu ya nyumbani kama upishi kunachochea mapenzi nyumbani.

“Mwanzo wa mawasiliano ni wakati wa mlo. Mambo mengine hufuata,” wanasema wataalamu wa tovuti hiyo.

Akiandika katika tovuti ya The Hindu Times, Mwanasaikolojia Ashariah Parween anasema wanaume wanafaa kuwapikia wake zao ili kuongeza furaha katika ndoa.

“Nyakati zimebadilika na japo ninasadiki upishi ni kazi ya wanawake, wanaume wanaotaka kuwa na ndoa zenye furaha hupika nyumbani,” asema.

Bw Okwemba asema ndoa inahusu wawili na wanafaa kusaidiana nyumbani kwa sababu haiwezi kuwa ndoa bila mmoja wao.

“Ndoa huwa inadhihirika nyumbani, sio mitaani. Inaweza tu kufaulu nyumbani kwa kusaidiana majukumu bila kusahau kilele ni chumbani,” asema.

You can share this post!

PENZI LA MAUTI: Mume na mpango wa kando wazuiliwa kwa...

Pasta aonya mwanawe asipotoshe vidosho kanisani

adminleo