Hasira zilivyompanda Kinyanjui akikanusha madai ya kutupa chokoraa msituni ‘kusafisha mji’
WAZIRI mteule wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda Lee Kinyanjui alipandwa na hasira alipokumbushwa kuhusu madai yaliyotolewa 2020 kwamba aliwakusanya chokoraa katikati mwa jiji hilo na kuwatupa ndani ya msitu wa Embobut ulioko Elgeyo Marakwet.
Akiwa mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi kupigwa msasa kubaini ufaafu wake kwa wadhifa huo, Gavana huyo wa zamani wa Nakuru alikumbushwa kuhusu suala hilo na Mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood.
“Kama mwenyekiti wa muungano wa watetezi wa watoto wanaorandaranda barabarani nchini ningependa kukuuliza ikiwa ni kweli kwamba uliwatupa watoto hawa katika msitu wa Embobut kama sehemu ya mpango wako wa kusafisha mji wa Nakuru ili upandishwe hadhi kuwa jiji?” Bw Dawood akauliza Jumanne, Januari 14, 2025.
Huku akionekana mwenye hasira, Bw Kinyanjui alijibu kwamba hayo yaliyokuwa madai yaliyotolewa katika bunge la Seneti na hasidi wake wa kisiasa wakati huo.
“Hayo yalikuwa madai tu; yaliletwa na mtu aliyekuwa na nia ya kuwa gavana. Hata mimi pia niko huru kutoa madai kuhusu watu wengine! Mheshimiwa Dawood hii ni propaganda chafu inayolenga kuniharibia jina bila sababu,” akasema.
Bw Kinyanjui alishangaa ni kwa nini mwanasiasa aliyeibua madai hayo ndiye mtu wa pekee katika kaunti Nakuru aliyeweza kupata habari kama hizo.
“Mbona hamna familia zilizojitokeza kudai kuwa wapendwa wao walipotea?” akauliza.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo, aliingilia kati na kumshauri Bw Kinyanjui awe mtulivu na asipandwe na hasira.
“Mheshimiwa Dawood alisema wazi kwamba hayo yalikuwa madai tu yaliyotolewa katika Seneti na yanasalia kuwa madai. Haimaanishi ni kweli kwamba uliwasomba chokoraa kwa malori ya tipa na kuwatupa ndani ya msitu wa Embobut wenye fisi na wanyama wengine hatari,” Bw Wetang’ula akaeleza.
Mwishoni mwa kikao hicho, kilichoendeshwa katika Ukumbi wa County, Nairobi, Spika huyo alimshauri Bw Kinyanjui kusoma kitabu chenye kichwa, “Namna ya Kufeli katika Mahojiano ya Kazi”. Bw Wetang’ula kulingana na kitabu hicho, mojawapo ya njia hizo ni “kupandwa na hasira”.