Ufisadi umekita mizizi Kenya – Ripoti
Na VALENTINE OBARA
UFISADI katika mashirika ya umma ungali juu licha ya hatua kali zilizochukuliwa na utawala wa Rais Uhuru Kenyatta kupambana na jinamizi hilo kwa mwaka mmoja sasa, utafiti umeonyesha.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na shirika la Transparency International (TI) iliyotolewa jana, ilionyesha Kenya ilikuwa na uadilifu wa asilimia 27 pekee katika taasisi za umma kufikia mwishoni wa 2018. Katika mwaka wa 2017, Kenya ilikuwa na alama 28 chini ya 100.
Rwanda ilikuwa na uadilifu zaidi Afrika Mashariki kwa asilimia 56 ikifuatwa na Tanzania (asilimia 36) huku Uganda ikiwa sawa na Kenya kwa asilimia 27. Burundi ilipata asilimia 17.
“Kenya iko katika nafasi ya 144 kati ya nchi 180 zilizochunguzwa. Matokeo ya Kenya ni ya chini mno ikilinganishwa na alama ya 43 iliyo wastani ulimwenguni na wastani ya 32 kusini mwa jangwa la Sahara,” shirika la TI nchini likasema kwenye taarifa.
Tangu Rais Kenyatta alipoingia mamlakani kwa hatamu ya pili ya uongozi, vita dhidi ya ufisadi vimepewa uzito hasa kuanzia wakati alipoweka muafaka wa maelewano na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga aliyeahidi kushirikiana naye katika juhudi hizo.
Kufikia sasa kesi za ufisadi zinaendelezwa dhidi ya washukiwa wengi wakiwemo maafisa wakuu waliotumikia mashirika ya umma kama vile Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), Kenya Pipeline, Kenya Power, Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) miongoni mwa mengine.
Hata hivyo, Idara ya Mahakama inayosimamiwa na Jaji Mkuu David Maraga, imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha au hata kuachilia huru washukiwa.
Lakini Jaji Maraga ameendelea kutetea afisi yake na kusema wao hutegemea ushahidi unaowasilishwa na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji inayoshirikiana na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Mkurugenzi Mkuu wa TI-Kenya, Bw Samuel Kimeu jana alisema ni sharti changamoto zote zinazokumba asasi hizo ikiwemo uhaba wa fedha zitatuliwe ili vita dhidi ya ufisadi vizae matunda.
“Afisi ya Rais huendelea kutoa matamshi makali dhidi ya ufisadi lakini hatujaona matokeo. Inahitajika ahadi ifuatwe na vitendo,” akasema.
“Baadhi ya asasi muhimu katika vita dhidi ya ufisadi zimekumbwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wa majukumu yao hasa kwa sababu ya jinsi wanasiasa na mabwenyenye walivyokita katika desturi ya kukwepa adhabu za kisheria,” akasema Bw Kimeu.
Shirika hilo lilitoa mapendekezo mbalimbali kubadili hali hii ikiwemo kutaka viongozi na watumishi serikalini kutangaza utajiri wao kidijitali ili iwe wazi kwa umma, na pia kuwepo sera mwafaka itakayoongoza jinsi wanasiasa na vyama vyao wanavyochanga pesa za kufanya kampeni.