Wakazi walia mkandarasi akiacha mifupa ya binadamu barabarani
WAKAZI wa Usonga katika Kaunti-ndogo mpya ya Siaya Magharibi wamelaumu maafisa wa serikali kwa kukosa kuondoa mifupa ya binadamu ambayo ilitupwa na mkandarasi anayekarabati barabara ya Lunyu – Kogoya.
Kulingana na wakazi hao, wamekuwa wakizuru afisi zote za serikali ya kitaifa na ya kaunti ya Siaya kwa takriban miezi miwili sasa bila suluhu huku mifupa hiyo ya binadamu iliyotupwa ikitapakaa.
Wakiongozwa na Alfred Ouma ambaye ua wa boma lake unapakana na barabara hiyo, wakazi hao walitaka uchunguzi ufanywe ili kubaini ulikotoka mchanga uliotumika kwenye barabara hiyo na ikiwa mabaki hayo ni ya mtu mmoja au watu kadhaa.
Ouma anasema kuwa serikali ya Kaunti ya Siaya haiwezi kukwepa lawama kwani ndiyo iliyompa mkandarasi huyo kazi ya kutengeneza barabara.
Anasema mkandarasi huyo alipoweka rundo la mawe pembeni mwa geti lake, mabaki ya mifupa ya binadamu yalionekana, hali iliyomlazimu kupeleka malalamishi yake kwa mkandarasi huyo ambaye alimpuuza.Anasema hata aliripoti kwa chifu wa eneo hilo ila hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Ouma anasema kwamba baadaye, mchanga ulisambazwa, na kutawanya mifupa si tu kwenye lango lake, bali pia kando ya barabara.
“Unaishi vipi na mabaki ya binadamu karibu na lango lako; mabaki ya mtu usiyemjua?” aliuliza.Alitoa wito kwa Waziri wa Masuala ya Ndani, Kipchumba Murkomen kuingilia kati haraka na kuamuru si tu kuondolewa kwa mifupa hiyo, lakini pia mchanga wote uliotumiwa, akiongeza kuwa familia yake imekuwa ikiota ndoto za kutisha kutokana na mabaki hayo.
Maoni yake yanaungwa mkono na Maureen Atieno aliyesema kwamba huwa inatisha watu wazima na watoto wanaopaswa kuvumilia kuona mifupa hiyo wanapofanya kazi zao za kila siku.
“Inasikitisha kwamba wakati wowote unapotembea kwenye barabara hii na kuona mifupa, kinachokuja akilini mwako ni kwamba unakanyaga wafu,” alisema na kuongeza kuwa kutojali kwa maafisa wa serikali ya Kaunti ya Siaya na wenzao wa serikali ya kitaifa kunatiliwa shaka.
Mwanakijiji, Vincent Owino anasema uamuzi wa maafisa hao kutochukua hatua uliashiria kwamba huenda maafisa wa serikali ya kaunti hiyo hawakuwa na uwezo au walihongwa na mkandarasi ili wapuuze masaibu ya wananchi.“Wasimamizi wa barabara walikuwa wapi? Je, ni lazima tumuachie gavana kila kitu,” aliuliza Owino na kuongeza:
“Ni mwiko kutupa mabaki ya binadamu kwenye lango la mtu.”