Habari za Kitaifa

Mkenya ashtaki X ya Elon Musk akidai inamomonyoa maadili ya jamii

Na  SAM KIPLAGAT January 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mkenya mmoja ameshtaki mtandao wa kijamii  wa X, akiilaumu kampuni hiyo ya Amerika kwa kuruhusu uchapishaji wa maudhui anayodai yanajumuisha matamshi ya chuki, uchochezi na uendelezaji wa ponografia, miongoni mwa shutuma zingine.

Bw Felix Kibet pia anashutumu  mtandao huo unaomilikiwa na bwanyenye Elon Musk kwa kuruhusu uchapishaji wa maudhui ambayo hayaheshimu haki na sifa za wengine.

Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye mnamo Jumatatu aliidhinisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuagiza Bw Kibet kukabidhi pande zote zilizotajwa kama washtakiwa stakabadhi za kesi, kabla ya kusikizwa kwa kesi hiyo Januari 17.

Bw Kibet anasema katika kesi yake kwamba kutowajibika kwa X kumewafanya Wakenya wa rika zote kuteseka na wanaendelea kuteseka kufuatia ukiukaji wa haki zao za kikatiba na kumomonyoka kwa maadili ya umma.

Machapisho katika X, anasema, ni tishio kwa muundo wa jamii ya Kenya.

“Mlalamishi anaamini kwamba mshtakiwa wa kwanza (X) katika kuruhusu, kuhimiza, kukubali na au kukuza katika jukwaa lake la kijamii la “X” (zamani Twitter) uchapishaji na ufikiaji nchini Kenya wa maudhui ambayo hayaheshimu haki na sifa nyingine ni kinyume cha Ibara ya 10 na 19 (3) ya Katiba,” anasema katika kesi yake.

Bw Kibet anaomba maagizo kadhaa— ikiwa ni pamoja na agizo la kumshinikiza Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor kuchukua hatua ambazo zitahakikisha  mitandao ya kijamii nchini inatii katiba na usalama wa Wakenya.

Anashutumu Mwanasheria Mkuu, Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA), Bodi ya Uainishaji wa Filamu ya Kenya na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kwa kukosa kutekeleza majukumu yao ya kikatiba na kisheria na badala yake kusalia kimya, kuunga mkono vitendo haramu  vya X, kinyume na Katiba.

Bw Kibet anasema kampuni hiyo kubwa ya mitandao ya kijamii kwa lengo ya  kujinufaisha, inaruhusu au kuhimiza uchapishaji na ufikiaji wa maudhui ambayo yanakiuka faragha ya Wakenya.

Katika kesi yake ya dharura, Bw Kibet anataka X kuzuiwa isiruhusu uchapishaji na ufikiaji wa maudhui yanayoonyesha au kutangaza ponografia, uchi na uasherati.

Pia anataka agizo kampuni hiyo isitishe uchapishaji na ufikiaji wa maudhui ambayo yanajumuisha matamshi ya chuki, uchochezi, utetezi wa chuki, kuwatukana wengine au uchochezi unaoweza kusababisha madhara katika mitandao ya kijamii.

Mtumiaji huyo wa mitandao ya kijamii anasema X inawaruhusu watumiaji kuwa na akaunti kwa kutumia lakabu au majina yasiyo rasmi, au majina na picha za watu wengine.

Bw Kibet anaendelea kusema X imeruhusu machapisho ambayo yanafichua bila sababu habari kuhusu masuala ya kibinafsi ya  Wakenya  na familia zao.

“Amri ya kudumu itolewe ili kumzuia mshtakiwa  wa kwazna kuruhusu uchapishaji au ufikiaji wa machapisho yaliyopingwa katika kesi ndani ya eneo la Jamhuri ya Kenya,” asema.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA