Magonjwa ya moyo na mapafu yazidi kuangamiza wengi
MAGONJWA ya moyo (CHD), kiharusi na ya mapafu, yamesalia kuwa kiini kikuu cha vifo duniani kote kwa miaka minne iliyopita, kulingana na uchambuzi wa takwimu.
Uchanganuzi wa Orodha ya Matarajio ya Afya Ulimwenguni- hifadhidata ya afya na umri wa kuishi duniani, ulifichua kuwa magonjwa haya yalichangia vifo vya watu milioni 4.5 mnamo 2020, na kuongezeka hadi milioni 77.9 mnamo 2024.
Ongezeko hili la kutisha linawakilisha mgogoro unaoongezeka wa afya duniani, unaochangiwa zaidi na mitindo ya maisha kama vile vyakula visivyofaa, kutofanya mazoezi, kuvuta sigara na shinikizo la damu lisilotibiwa au kisukari.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linafafanua ugonjwa wa moyo kama hali ambayo hutokea wakati mishipa ya damu ambayo husafirisha damu yenye oksijeni kwa misuli ya moyo, inapungua au kuziba kutokana na mkusanyiko wa mafuta.
Kuziba huku kunapunguza mtiririko wa damu kwenye moyo na kunaweza kusababisha maumivu ya kifua, mshtuko wa moyo au matatizo mengine makubwa ya moyo.
Nchini Kenya, hali inaakisi hali ya kimataifa, huku ugonjwa wa moyo na mishipa ukiibuka kuwa chanzo kikuu cha vifo. Masuala kama vile kuongezeka kwa miji, lishe duni na ukosefu wa mazoezi yamechangia kuongezeka kwa hatari kama vile unene, shinikizo la damu na kisukari.
Vilevile, upatikanaji wa huduma za afya bado ni changamoto kubwa, hasa katika maeneo ya vijijini ambako vifaa vya uchunguzi na matibabu ni vichache.Hospitali nyingi za umma hazina rasilimali za kuyadhibiti magonjwa ya moyo na mishipa, na uelewa wa hatua za kuyazuia bado ni mdogo.
“Kuna hitaji la dharura la kampeni za afya ya umma za kimakusudi, uwekezaji katika miundomsingi ya huduma za afya na kuboreshwa kwa upatikanaji wa huduma ili kukabiliana na tatizo hili linaloongezeka,” alisema Dkt Evans Bosire, mshauri wa magonjwa ya moyo.
Ugonjwa wa kiharusi (stroke), ambao ni wa pili kwa kusababisha vifo vingi duniani, ulionyesha ongezeko kubwa kutoka takriban vifo milioni 1.5 mwaka wa 2020 hadi vifo milioni 26.4 mwaka wa 2024, jambo linalosisitiza kuongezeka kwa mzigo wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs), ambayo sasa huua watu wengi zaidi kuliko magonjwa ya kuambukiza katika nchi nyingi.
Nchini Kenya, ugonjwa wa kiharusi unazidi kuwa tatizo kubwa la kiafya, hasa kutokana na viwango vya juu vya shinikizo la damu na kisukari. Kugunduliwa mapema, elimu na matibabu ya hali hizi yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyohusiana na kiharusi.
Takwimu zinaonyesha kuwa kiharusi kinasalia kuwa chanzo kikuu cha vifo nchini Kenya, huku kiwango cha vifo kikiwa watu 92 kwa kila watu 100,000, ikishikilia nafasi ya 81 duniani, huku zaidi ya vifo 25,000 vikiwa vimetokana na uhaba wa madaktari wa mfumo wa neva na huduma za dharura za matibabu.
“Kugunduliwa mapema kwa kiharusi ni muhimu katika kuboresha matokeo ya mgonjwa. Wakati ni muhimu katika matibabu yake. Kama nchi, tuna mahitaji makubwa katika eneo hili na pengo kubwa lipo linalopaswa kutatuliwa kwa kutoa fursa za mafunzo,” alisema Dkt Tasneem Yamani, daktari wa watoto katika Hamat Healthcare.
Ugonjwa wa mapafu, ambao ni chanzo cha tatu cha vifo, pia unachangia ongezeko kubwa la vifo, kutoka kwa vifo 795,913 hadi vifo milioni 13.7m katika kipindi hicho. Ongezeko hili linahusishwa na mambo kama vile uchafuzi wa hewa, uvutaji sigara na magonjwa ya kupumua. Ugonjwa huu unaua Wakenya kwa kiwango cha 26.82 kwa kila watu 100,000.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA