Mwanajeshi aliyetekwa na Shabaab kambini El Adde 2016 yuko hai
MIAKA tisa iliyopita, familia ya Abdullahi Issa Ibrahim, afisa wa KDF aliyetekwa nyara na Al-Shabaab wakati wa shambulizi katika kambi ya El Adde, ilikata tamaa ya kumuona akiwa hai na kufikia hatua ya kufanya ibada ya mazishi kulingana na imani za Kiislamu.
Lakini Jumatano, miaka tisa baada ya shambulio hilo la 2016 na kutekwa nyara kwake, familia ya Ibrahim ilipokea kwa furaha ripoti kwamba jamaa yao alikuwa hai kupitia mawasiliano ya simu naye na video iliyodaiwa kutumwa kwenye mitandao ya kijamii na wanamgambo wa Al Shabaab.
Kupitia video hiyo, familia inasadiki kuwa jamaa yao yuko hai mikononi mwa watekaji nyara hao. “Kama familia tulikuwa na hakika kwamba aliuawa miaka sita iliyopita, lakini tulipoona video sasa tuna uhakika kwamba yu hai,” alisema Katra Abdullahi, binti wa sajini huyo wa KDF.
Akizungumza na wanahabari mjini Eldoret nyumbani kwa afisa huyo aliyetekwa nyara, katika mtaa wa Maili Nne, Bi Katra alisema video hiyo ilikuwa ya babake ambaye alimtambua bila kubahatisha.
Bi Katra alisema kabla ya video hiyo kutolewa alipokea simu kutoka kwa babake ambaye alimwambia kwamba alikuwa hai.
Bi Katra alisema wakati wa mazungumzo na babake alimwomba awaombe watekaji wake watumie familia video yake ya sasa.
Babake alimwambia kuwa watekaji wake wangetuma video hiyo kupitia vyombo vyao vya habari. Hatimaye walituma video hiyo ambayo imeifanya familia hiyo kuamini kuwa jamaa yao bado yuko hai.Kwa sasa familia hiyo inaomba serikali kuisaidia kumrejesha nyumbani.