Uhuru hatawasaidia, Ruto aambia vijana akiwataka watafute ajira katika miradi ya serikali yake
RAIS William Ruto amewataka vijana kuwapuuza viongozi wanaowachochea kuzua fujo na uharibifu wa mali bali wajipange kupata ajira katika miradi na mipango ya serikali yake.
Aliwaonya viongozi hao kukoma kuwachochea vijana kushiriki maandamano ila akawataka wawaelekeze ili waweze kujiendeleza.
“Vijana wanahitaji mazuri kutoka kwetu kama viongozi. Kwa hivyo, kama viongozi tusiwachochee ili washiriki maandamano ya fujo,” Dkt Ruto akasema Jumapili.
Rais aliwahimiza vijana kukataa ushauri wa viongozi kama hao na wajiandae kufaidi kutokana na mipango na miradi ambayo serikali inatekeleza kwa ajili ya kuwapa nafasi za ajira.
“Muwakatae wale wanaowachochea mfanye maandamano kwani hawana mipango ya kuwasaidia. Mtafute ajira kupitia mipango kama vituo vya kidijitali vilivyoko katika wadi zote chini, mpango wa serikali wa kuwatafutia Wakenya ajira ng’ambo, mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na mradi ambayo serikali inaendesha ya kujenga masoko 400 kote nchini,” Dkt Ruto akaeleza.
Rais, ambaye alikuwa akihutubu wakati wa Ibada ya Pamoja ya Jumapili katika eneo la Cheptais, eneobunge la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma, alionekana kumlenga Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye juzi alitaka vijana wa Gen Z kuendelea kupigania haki yao na utawala bora bila woga.
Hata hivyo, hakumtaja moja kwa moja bali alimtaka atoe mpango mbadala wa kuwasaidia vijana badala ya kuwachochea vijana washiriki fujo.
Rais Ruto alieleza kuwa serikali yake imetoa nafasi 180,000 za ajira chini ya mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na nafasi zingine 250,000 chini ya mpango wake wa kuwafutia Wakenya ajira ughaibuni.
Mnamo Ijumaa wiki jana Bw Kenyatta aliwashangaza wengine alipotoa wito kwa vijana wa Gen Z na wengine kuendelea kupigania haki zao na bila woga. Alielezea kujitolea kwake kuwaunga mkono vijana katika juhudi hizo.
“Shida ya wengine ni kusambaza woga. Hamna kitakachodumu milele. Nyinyi Gen Z ndio tegemeo la miaka ijayo. Kwa hivyo, mpiganie haki zenu. Msiketi tu mkitizama yote mliofanyia kazi ikichukuliwa…… msikubali jambo kama hilo. Msimame kidete na mhakikishe mnapata haki yenu…….sisi tuko nyuma yenu na tutawaunga mkono,” akasema.
Bw Kenyatta alisema hayo wakati wa ibada ya mazishi ya binamuye, Kibathi Muigai, katika kijiji cha Ichaweri, Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu.
Lakini, jana, akionekana kujibu kauli hiyo, Rais Ruto aliwataka viongozi kuunga mkono mipango ya serikali yake ya kuwasaidia vijana “badala ya kuwapiganisha na serikali.”
Baadhi ya wabunge kutoka kaunti hiyo ya Bungoma waliohutubu kabla ya Rais Ruto, walimwonya Bw Kenyatta dhidi ya kuwachochea vijana wa Gen Z na kuikosea serikali hii ya Kenyatta.
Mbunge wa Sirisia John Waluke na mwenzake wa Webuye Magharibi Daniel Wanyama walimtaka Bw Kenyatta kutulia na kuendelea kupokea malipo yake ya uzeeni.
“Ni makosa kwa Uhuru kuwaambia vijana warudi barabarani kupambana na serikali. Ikiwa nchi hii itachomeka watu wote wataathirika akiwemo yeye licha ya kwamba amestaafu,” akasema Bw Waluke.
“Nawataka vijana kumpuuza Uhuru na waunge mkono serikali ya Rais William Ruto kwa sababu imeratibu mipango mizuri ya kuwasaidia,” akaongeza mbunge huyo, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge kutoka Magharibi mwa Kenya.
Kauli ya Bw Kenyatta imeibua hisia mseto nchini huku wengine wakiifasiri kama iliyolenga kuishambulia serikali ya Rais Ruto.
Rais huyo mstaafu alitoa kauli hiyo mwezi moja baada ya kuonekana kuiunga mkono utawala wa Dkt Ruto kufuatia kuteuliwa kwa wandani wake kuwa mawaziri.
Wao ni; Mabw Mutahi Kagwe (Waziri wa Kilimo), William Kabogo (Waziri wa ICT) na Waziri mpya wa Biashara Lee Kinyanjui.
Watatu hao waliteuliwa mnamo Desemba 18, 2024, siku chache baada ya Rais Ruto kumtembelea Bw Kenyatta nyumbani kwake katika kijiji cha Ichaweri, Kaunti ya Kiambu.