Habari

Watu 70 walazwa hospitalini wakiugua baada ya kunywa mursik kwenye hafla ya kanisa

Na  WINNIE CHEPKEMOI January 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya watu 70 kutoka vijiji vya Kabianga na Masaita, Londiani Mashariki Kaunti ya Kericho Jumapili walilazwa hospitalini baada ya kunywa maziwa aina ya mursik kwenye hafla ya kanisa.

Watu hao ambao walihudhuria hafla ya kufuzu kanisani, wanaendelea kutibiwa kwenye Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Londiani.

Mursiki ni maziwa yaliyoganda yaliyohifadhiwa vizuri, yana uchachu na yana umuhimu wa kitamaduni miongoni mwa jamii ya Kalenjin.

Walioathirika wakiwemo watoto 12, walikuwa wakitapika na kuharisha baada ya kunywa maziwa hayo,

Mkurugenzi wa Chuo cha Mahubiri, Kericho ambako hafla hiyo ilikuwa ikiandaliwa alisema walinunua mursik hiyo mnamo Ijumaa kutoka kwa muuzaji rejareja kabla ya hafla yenyewe. Walikuwa wakitarajia zaidi ya wageni 20 kuyanywa maziwa hayo.

Muuzaji huyo ameenda mafichoni baada ya kupata habari kuwa polisi walikuwa wakimsaka aandikishe taarifa kuhusiana na tukio hilo.

“Tulienda kijijini kununua mursik ambayo huwa ina uchachu na tukapata maziwa hayo kabla ya sherehe yenyewe,”  akasema Bw Korir.

Saa chache baada ya kuyanywa, waliohudhuria walianza kuhisi maumivu ya tumbo, baadhi wakitapika na kuendesha. Madaktari katika hospitali ya Londiani walikuwa na wakati mgumu kuwahudumia waliokunywa maziwa hayo.

Zaidi ya watoto 12 walilazwa wakiwemo 12 kutoka familia mmoja na walikuwa wamedungwa maji yenye dawa ili kuwapunguzia maumivu.

Mmoja wa walioathirika Paul Korir alisema alianza kutapika na kuendesha baada ya kunywa maziwa hayo na akalazimika kuenda kusaka matibabu. Alisema alishangazwa na ubora wa maziwa hayo kwa sababu mwanamke aliyewauzia alikuwa ameshiriki biashara hiyo kwa kipindi kirefu.

Bi Betty Kirui, mama wa watoto sita alisema wanawe wawili waliathirika vibaya na walikuwa wamelazwa wakiwa hali mbaya kiafya.

“Nashukuru watoto wangu wanne walikuwa shuleni na hawakuhudhuria sherehe hiyo. Mimi na mume wangu hatukuwa na bahati kwa kuwa tulikunywa maziwa hayo na sasa mimi ni dhaifu siwezi kutembea. Pia nina wasiwasi kuhusu hali ya watoto wangu wawili,” akasema Bi Kirui.

Muuguzi Morine Chepkoech alisema watoto wengi ndio waliathirika na akawataka wazazi wajihadhari na chakula au vinywaji wanavyovitumia kwenye hafla za umma.

Polisi na machifu wanaendelea na uchunguzi kuhusu kisa hicho.