Siasa

NI KUPAA TU: Mbadi, Wandayi wajaza anga ya Luo Nyanza kwa helikopta

Na GEORGE ODIWUOR January 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TANGU maafisa wa zamani wa ODM John Mbadi na Opiyo Wandayi wateuliwe mawaziri Julai mwaka jana wamekuwa wakisafiri kwa ndege kutembelea sehemu mbalimbali za Luo Nyanza.

Kabla ya hapo anga ya eneo hilo ilikuwa safari za ndege zilikuwa chache zaidi, isipokuwa ndege za kibiashara.

Lakini nyakati hizi, anga ya Luo Nyanza iko na shughuli nyingi hasa wikiendi kwani helikopta za kibinafsi hupaa kila mara zikiwa zimewabeba mawaziri hao na wanaondamana kwenye safari zao.

Mawaziri Mbadi (Fedha) na Wandayi (Kawi) hutembelea maeneo mbalimbali Luo Nyanza wakielezea mipango ya serikali hasa siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Mabw Mbadi na Wandayi, ni miongoni mwa viongozi ambao wameachana kutuma magari na kuamua kutumia helikopta kusafiria, ishara ya kudhihirisha eneo hilo sasa lipo sawa sawa serikalini.

Awali, Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Afisi ya Rais Eliud Owalo ndiye alikuwa akizuru maeneo mbalimbali ya Luo Nyanza kwa kutumia helikopta siku za wikiendi.

Alipohudumu kama Waziri wa ICT na Uchumi wa Kidijitali, Bw Owalo aliweka rekodi ya kuzuru maeneo mbalimbali kwa kutumia helikopta.

Nyakati nyingine alikuwa akitumia helikopta ya kijeshi kutembelea maeneo hayo akisambaza chakula cha msaada kwa wahanga wa mafuriko katika kaunti za Migori, Homa Bay na Kisumu.

Baadhi ya wakosoaji wa Owalo walimsuka kwa kuharibu pesa za umma kuzunguka kote Nyanza akisambaza chakula cha msaada.

Kando na mawaziri Mbadi na Wandayi, Katibu wa Wizara ya Usalama Raymond Omollo pia hupenda kutumia helikopta akitembelea maeneo mengi Kenya na hata Luo Nyanza.

Mwingine anayetumia helikopta ni Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga anayewania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Bw Wandayi na Bw Mbadi Ijumaa wiki hii walitumia helikopta tatu kusafiri hadi kijiji cha Manyala kilichoko eneobunge la Suba Kusini kuzindua mradi wa stima.

Ilisemekana kuwa wengi wa wakazi walikuwa wakiona helikopta kwa karibu na kufurahia maendeleo hayo mapya

Katibu wa Baraza la Wazee wa Suba ya Kati Joab Ikawa alisema ziara ya mawaziri hao kwa kutumia helikopta tatu ni ishara ya mamlaka na ukwasi wao ndani ya serikali.

“Kuwasili kwao kuliibua msisimko miongoni mwa wakazi. Watu hawajawahi kuona maafisa wa serikali wakiwasili kwa mtindo huu,” akasema.

Mzee Ikawa pia aliongeza kuwa mawaziri hao wawili wanaonekana kupata uungwaji mkubwa kutoka kwa Rais William Ruto.

Bw William Odhiambo, mkazi wa kijiji cha Manyala, alisema hajawahi kuona kijiji chake kikitembelewa na maafisa wakuu wa serikali wakitumia helikopta.