NIPE USHAURI: Natamani kuonja mjakazi wetu kisiri
NINA mke na nampenda sana, lakini nimekuwa nikimmezea mate mjakazi wetu. Kuna tatizo la kutaka kumuonja mradi mke wangu asijue?
Sio jambo la busara kuhatarisha ndoa yako eti kushibisha kiu cha muda mfupi. Pia, unahatarisha afya yako na mkeo kwani huko nje kuna maradhi ya zinaa.
Mume wangu anavutia mademu wengi mtaani
Mume wangu ni mtanashati na ana hela, jambo ambalo limemfanya kuwa kivutio cha vimada mtaani. Hii imekuwa ikinipa wasiwasi. Nifanye?
Macho hayana pazia na hivyo huwezi kuwazuia wanawake wengine wasimtambue. Jukumu lako ni kutimiza majukumu yako kama mke. Kwa upande wake, ikiwa anakupenda na kuheshimu ndoa yenu, hapaswi kutambua macho ya wengine.
Sitaki babangu aoe tena
Mamangu alitengana na babangu na kumuachia watoto watatu. Mimi ndiye kifungua mimba na tayari nimeoa, huku ndugu zangu wawili wangali chuoni. Hivi majuzi babangu alimtambulisha mwanamke fulani ambaye anapanga kumuoa. Mamangu alikoenda aliolewa na kupata familia ingine. Sikubaliani na uamuzi wa babangu kuoa.
Elewa kwamba babako pia ana hisia na ana kila haki ya kupendwa. Sio haki kutaka kumzuia ilhali wajua kwamba uhusiano wake na mamako ulikwisha.
Mume anapenda mzaha na wanawake kazini
Nimegundua kwamba mume wangu anafanya mzaha sana na baadhi ya wanawake kazini mwake. Nilijua haya baada ya kukumbana na jumbe za kiajabu katika simu yake, kutoka kwa wanawake kadhaa anaofanya kazi nao. Hasa mzaha wao ni kuhusu masuala ya ngono. Nifanyeje?
Kwanza unapaswa kujua kuwa ni makosa kusoma jumbe za mwenzio bila ruhusa. Hata hivyo, kwa sasa huna budi ila kumwambia mumeo kuhusu udhia wako kuhusiana na jumbe ulizokutana nazo. Ikiwa anakupenda na kuheshimu ndoa yenu, ataacha tabia hii mara moja.