Kioni: Serikali ilisambaza picha za Uhuru na Ruto wakisalimiana kama propaganda
KATIBU Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni amesema hakuna muafaka wowote uliopo kati ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na mrithi wake, William Ruto kwa lengo la kumsaidia ahifadhi kiti chake katika uchaguzi mkuu 2027.
Bw Kenyatta ndiye kiongozi wa chama cha Jubilee (JP), na kulingana na Bw Kioni, tetesi zinazoenezwa kuwa kuna handisheki baina ya Rais huyo wa nne wa Kenya na Dkt Ruto ni propaganda tu.
Kauli ya katibu mkuu huyo wa Jubilee, inajiri mwezi mmoja baada ya ziara ya ghafla ya Rais Ruto nyumbani kwa Bw Kenyatta, Ichaweri Gatundu, Kiambu.
Picha za wawili hao zilifichuka na kusambaa mitandaoni, wakionekana nyumbani kwa Mzee Jomo Kenyatta, Rais wa Kwanza wa Kenya, katika hali ya kukumbatiana – ishara ya kuzika tofauti zao za kisiasa.
Ziara ya Rais Ruto kwa Bw Kenyatta ilifanyika Desemba 2024, na ni hatua iliyoshtua wengi ikizingatiwa kuwa wanasiasa hao hawajakuwa wakipikika kwenye chungu kimoja kuanzia 2018.
Dkt Ruto alihudumu kama naibu wa rais kati ya 2013 na 2022, na Bw Kenyatta aliunga mkono kuchaguliwa kwa kiongozi wa ODM, Raila Odinga kwenye uchaguzi uliopita, hatua ambayo haikumridhisha Ruto.
Bw Kioni aliahidi jana kwamba rais mstaafu angali anathamini taifa na kwamba anatakia Wakenya mema.
“Anataka serikali inayoongoza nchi vyema, tulivu na inayofanikiwa,” mbunge huyo wa zamani Ndaragwa alisisitiza.
Aidha, aliwataka wafuasi wa JP kuendelea kuwa waaminifu kwa chama.
Kutokana na matamshi ya hivi majuzi ya Bw Kenyatta – kuunga Gen Z mkono waendelee kutetea haki zao, Kioni alisema ni ishara kuwa rais huyo wa zamani ana uwazi kwa ahadi zake kwa Wakenya.
Bw Kenyatta alitoa matamshi hayo mnamo Ijumaa, Januari 17, 2025 katika hafla ya mazishi ya binamu yake, Kibathi Muigai aliyezikwa Gatundu Kusini, Kiambu.
Rais huyo mstaafu alisikika akihimiza Gen Z kutolegeza kamba na kuendelea kutetea haki zao kupitia maandamano.
Kauli ya Bw Kenyatta, hata hivyo, imeonekana kumkera Rais Ruto, mnamo Jumapili, Januari 19 akimsuta kama kiongozi “anayechochea vijana dhidi ya serikali.”
Bw Kioni, pia, alikejeli tetesi kuwa Rais Ruto kwenye ziara yake Gatundu, alimpelekea Bw Kenyatta mbuzi 12 kama ishara ya kujaribu kuomba msamaha kutokana na tofauti zao kisiasa.
Wakati wa maandamano ya Azimio la Umoja mwaka 2023 dhidi ya serikali, shamba la familia ya Kenyatta eneo la Ruiru, Northlands City, lilivamiwa na wahuni, kondoo wake wakaibwa na sehemu kuchomwa.
Baadhi ya wanasiasa ambao ni wandani wa Ruto, walinyoshea kidole cha lawama Bw Kenyatta wakidai ndiye alikuwa akifadhili maandamano hayo, yakiwemo ya Gen Z.
Msimamo wa Jubilee, unajiri licha ya baadhi ya wandani wa Bw Kenyatta kujiunga na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Kenya Kwanza ambao ni; Mutahi Kagwe aliyeteuliwa na Ruto kuwa Waziri wa Kilimo na Ustawishaji Mifugo na aliyekuwa Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui (Wizara ya Biashara).
Aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo naye aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Teknolojia na Uchumi Dijitali.