Habari za Kaunti

Moto wazidi kuenea Isiolo huku ukiibua hofu kwa wakazi

Na DAVID MUCHUI January 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MOTO unaendelea kuteketeza mashamba katika Kaunti ya Isiolo sasa unachukuliwa kama tishio kubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambao ni wafugaji.

Moto huo ambao umeteketeza karibu ekari 200,000 katika eneo la Merti, umehusishwa na jaribio la wafugaji kupambana na kupe katika maeneo makubwa ya malisho.

Kamishna wa Kaunti ya Isiolo, Bw Geoffrey Omoding, Jumatatu alisema kuwa moto huo kufikia sasa umeharibu zaidi ya ekari 190,000. Alisema moto huo ulikuwa ukiendelea kuteketeza maeneo ya Bassa, Matarba na Sericho Jumatatu asubuhi.

“Tumewahamasisha wenyeji ambao wanajaribu kuzima moto huo asubuhi na jioni. Kwa sasa, tunatafuta mashine za kusaidia kuzima moto. Kwa bahati nzuri, moto hauko karibu na makazi,” Bw Omoding alisema.

Moto mkubwa zaidi umeripotiwa kuanza katika eneo la Malkagalla huko Merti wiki moja iliyopita na unaendelea kuteketeza nyasi, vichaka na miti.

Moto wa pili ulizuka Chaffa karibu na kinamasi cha Lorian, kando ya Mto Ewaso Nyiro, Sericho siku nne zilizopita.

Kulingana na Meneja wa Hifadhi ya Jamii ya Sericho Nura Halkana, moto huo umeharibu takriban hekari 28,000 za ardhi ya malisho katika eneo hilo. Hata hivyo, inakadiriwa kuwa zaidi ya hekari 16,000 zimeathirika.

“Moto huo ulisababishwa na wafugaji ambao walikuwa wakijaribu kuondoa kupe katika eneo la malisho. Kumekuwa na uvamizi mkubwa wa kupe na kuna watu wanaofikiri moto ndio tiba,” Bw Halkana alisema.

Bw Halkana alibainisha kuwa uharibifu wa eneo la malisho kama njia ya kuokoa wafugaji wakati wa kiangazi, huenda ukaleta athari kubwa kwa afya ya mifugo.

“Imekuwa vigumu kuuzuia moto huo kutokana na ukosefu wa vifaa hitajika. Takriban wakazi 100 wanajaribu kukabiliana na moto huo. Ikiwa malisho yataharibiwa, wanyama watateseka mwaka huu,” alisema.

Ukaguzi kwa kutumia ramani za kupitia mtandao wa Google pia unaonyesha kuwa moto kama huo wa nyika kwa sasa unawaka katika eneo la Leisanyu, Kaunti ya Wajir ambapo zaidi ya ekari 33,000, zimeathirika.

Pia eneo la Illeret katika Kaunti ya Marsabit (zaidi ya ekari 1,200), Suiyian katika Kaunti ya Samburu (zaidi ya ekari 1000) na Lorau huko Turkana (zaidi ya ekari 51,000).

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema wafanyakazi wao wamekuwa wakisaidia wenyeji na Maafisa za Wanyamapori katika kudhibiti moto wa Sericho kwa siku mbili zilizopita. Shirika hilo lilisema mashine spesheli zinatumika ili kudhibiti moto huo.

“Moto bado unawaka, ukisambaa kuelekea vijiji vya Sericho, Biliki, Badana na Basa. Tunajaribu tuwezavyo kuudhibiti usisambae zaidi,” ilisema taarifa ya shirika la Msalaba Mwekundu nchini.