Gumzo ‘toka Amerika: Acha nikwambie, ujio wa pili wa Trump unaburudisha sana!
SAMAHANI rafiki yangu, usinitumie video za Tiktok. Najua zinachekesha, na natamani kucheka hadi mbavu ziniteguke, lakini viungo vya video zako havifunguki kwenye simu yangu.
Tiktok ni marufuku ninakoishi, hivyo unaponengua viuno na kujirekodi ukitarajia nishabikie weledi wako huo unajichosha bure tu.
Hata hivyo, kuna matumaini. Tumepata mzee wa Nyumba Kumi, Donald Trump, na ameahidi ataangalia mambo yetu ili Tiktok ihalalishwe tena.
SOMA PIA: MAONI: Tusidanganyane, umaarufu wa Trump umechochewa na rangi yake na itikadi kali
Ilipigwa marufuku na Mahakama ya Upeo kwa kuwa inamilikiwa na Wachina, raia wa taifa la wapenzi wa udaku kwa mujibu wa Amerika, lakini Trump, kipenzi cha wafanyabiashara, amesema ana suluhisho.
Mwafrika Mweupe Elon Musk
Amemwambia tajiri mkuu duniani, Mwafrika mweupe aliyehamia Amerika, Elon Musk, anunue mtandao huo na kuwarejeshea Waamerika raha yao.
Hadi hilo litakalofanyika, tafadhali ukirekodi video zako ni bora uwatumie watu wenu ili wakupe maoni uliyotaka kutoka kwangu.
Hakikisha kwanza umewatumia wazazi wako ulizorekodi ukiwa nusu uchi ili nao wazione. Si ulitaka kunipotosha? Hata mimi ni mtoto wa watu.
Ngoja nikwambie, ujio wa pili wa Trump unaburudisha. Ametukumbusha Mungu aliumba jinsia mbili: kike na kiume.
Kwa bahati nzuri, naijua jinsia yangu vyema, hivyo sina haja kwenda pembeni kuhakikisha iwapo nahitaji kuwa mwangalifu ili nisiadhibiwe na Trump.
SOMA PIA: MAONI: Democrats wanafaa kujilaumu wenyewe kwa Kamala kufeli, hata ingawa Trump alitumia ujanja
Natafakari tu yanayoendelea katika maisha ya mtu anayedai… sijui keshabadili jinsia au yupo kati ya kike na kiume; mara anahisi kama amebanwa katika mwili wa jinsi hii ilhali yake ni ile… yaani msongamano ya mambo ya kipuuzi tu!
Najikuna kichwa na kujiuliza iwapo kweli Trump na utawala wake wametafakari kuhusu adhabu anayopaswa kupewa anayejitambulisha kwa jinsi isiyokuwa yake.
Hebu tutafakari mtu akifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka: “Ewe uliyekanganyikiwa kiasi cha kutojua jinsia yako, unashtakiwa kuwa mnamo tarehe fulani, mwezi fulani, ulionekana kuwa na tabia za kike, ilhali Trump anadhani wewe ni mwanamume.”
Halafu anaambiwa, “Unapaswa kuadhibiwa vikali mno, hasa kwa kuwa umemkasirisha rais, lakini kwa kuwa wewe ni mkosaji wa kwanza, mahakama hii inakupa onyo: Acha umama au usenge!”
Watu wanakucheka, unaondoka na kujiendea zako, halafu unaanza safari ya kuigiza kuacha ‘umama’ au ‘usenge’, ambao tangu mwanzo ulianza kuigiza na ukakaribia kufaulu, ghafla Trump akarejea Ikulu.
Nguvu ya kushiriki utoto
Katika dunia hii ambapo maradhi, njaa na ujinga ni changamoto kuu, watu wanatoa wapi nguvu za kushiriki utoto kiasi hicho? Nalaumu ujinga.
Hata hivyo, lazima niseme wazi kwamba upuuzi huo wa watu kuhisi namna fulani na kuamini ndivyo walivyo ni njama ya ibilisi kutupeleka jehanamu. Hataki kuteketea peke yake.
SOMA PIA: MAONI: 2025 heri Afrika ijipange kwa sababu hakuna atakayeshughulika na matatizo ya bara hili
Kumhusu Trump, jiandae kucheka. Akijenga ukuta na kuwazuia wahamiaji haramu wanaoingia Amerika kutoka Mexico huku wakileta dawa za kulevya, waraibu kutoka Amerika watauvunja ukuta wenyewe wakielekea Mexico kuzifuata.
Kalia jamvi tutizame kioja. Mradi Trump anapumua, kusinzia ukitazama habari ni ishara kwamba umeng’atwa na mbung’o ukaambukizwa malale. Amka!
– Douglas Mutua ni mwanahabari na mwandishi anayeishi Amerika, jimbo la Virginia
Mpate katika: [email protected]