Kinachofanya watu kukataa uteuzi serikali ya Rais Ruto
IDADI ya watu wanaokataa kazi wanazoteuliwa kushikilia serikalini inaonyesha kuwa watu wengi wamekosa imani na utawala wa Kenya Kwanza wakilenga kuokoa hatima zao za kisiasa.
Baadhi ya wale ambao wamekataa uteuzi wa Rais William Ruto katika nyadhifa za serikali kufikia sasa ni wanasiasa wenye uzoefu, wanaojulikana kwa misimamo yao na wataalamu wa sekta mbalimbali.
Japo uteuzi huo unalenga kuzawadi wanaochukuliwa kuwa waaminifu kwa utawala wa sasa pamoja na washirika wapya wa Rais Ruto katika Serikali Jumuishi- Raila Odinga na kwa kiasi fulani Uhuru Kenyatta- wachanganuzi wanasema wengi wanahisi kuwa utazika ndoto zao za kisiasa.
“Wale wanaofuatilia hali halisi mashinani na hisia za wapigakura hawawezi kukubali wadhifa katika serikali hasa kutoka maeneo ambayo mwelekeo wa kisiasa unakinzana na sera za Kenya Kwanza,” asema mchanganuzi wa siasa, Dkt Isaac Gichuki.
Anasema kwamba kuna wale wanaohisi kuwa kazi wanazopewa ni duni kuliko za kifahari walizotarajia hasa baada ya kuunga chama tawala katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.
Wale ambao wamekataa kazi za Ruto katika miezi ya hivi majuzi ni pamoja na aliyekuwa waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Uchumi Dijitali Margaret Ndung’u na mweka hazina wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Timothy Bosire.
Dkt Ndung’u ambaye aliteuliwa waziri wakati Ruto alipounda baraza la pili la mawaziri alikuwa ameteuliwa balozi wa Kenya nchini Ghana. Katika barua aliyoandikia kamati ya bunge iliyosubiri kumpiga msasa, Dkt Ndung’u alitaja sababu za kibinafsi na kifamilia kama kiini.
Bw Bosire aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) wadhifa ambao alikataa baada ya kushauriana kwa mapana.
Kabla ya wawili hao kukataa kazi walizoteuliwa na rais, aliyekuwa Seneta Mteule Millicent Omanga na aliyekuwa mbunge wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi pia walikuwa wamekataa kazi walizopewa na Ruto.
Omanga na Kemosi, walikuwa msitari wa mbele kufanyia UDA kampeni kabla ya uchaguzi wa 2022. Omanga alikataa uanachama wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kenya Shipyards, huku Kemosi akikataa kuwa Balozi wa Kenya nchini Ghana.
Wawili hao pia walitaja sababu za kibinafsi kuwa kiini. Kulingana na Dkt Francis Kalaa, mchanganuzi wa siasa na utawala, Bi Omanga na Kemosi walihisi kudunishwa hasa baada ya kufanyia kazi chama cha UDA zaidi ya baadhi ya watu waliotunukiwa nafasi kubwa serikalini.
Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo alikataa uteuzi wa Ruto kuwa mwanachama wa jopokazi huru la kukagua deni la Kenya.
Bi Odhiambo alisema kuteuliwa kwake kuwa mwanachama wa jopo la kukagua deni la nchi kulikiuka sheria kwa kuwa kazi ya kukagua deni la kitaifa ni jukumu la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Aliyekuwa mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka, mwaka jana alikataa uteuzi wa kuwa mwenyekiti wa bodi ya shirika la serikali akisema kuwa utawala wa sasa umepoteza mwelekeo.
“Baada ya mashauriano ya kina na kwa kuzingatia hali ya sasa ya kisiasa ambayo inatishia kutekelezwa kwa ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi ya Serikali, nimefanya uamuzi mgumu wa kukataa uteuzi huu,” Dkt Munyaka alisema katika taarifa.Kabla ya uteuzi huo, Munyaka ambaye aliwakilisha eneobunge la Machakos Mjini kwa mihula mitatu alikuwa amesuta serikali kwa kutenga eneo la Ukambani.
“Ingawa matamshi yangu yanaweza kusawiriwa kuwa uasi, lazima nimweleze rais ukweli: tunahitaji huduma na ajira kwa watu wetu,” Munyaka alisema alipokuwa akiwahutubia waombolezaji katika eneobunge la Mavoko mwaka jana.
Dkt Kalaa anasema ukweli ni kwamba umaarufu wa serikali ya Kenya Kwanza umeshuka hasa kutokana na sera zake za ushuru mwingi, kupuuza kilio cha raia na ukatili wa maafisa wa usalama wanaohusishwa na utekaji nyara.
“Hali hii imefanya walio na ndoto za kugombea viti vya kisiasa kufuatia hisia za wakazi huku wataalamu wakiepuka kujipaka matope ya kisiasa,” akasema.