Jamvi La Siasa

Gachagua na Kindiki wanavyopimana ubabe

Na BENSON MATHEKA January 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

NAIBU Rais Kithure Kindiki na mtangulizi wake Rigathi Gachagua wanaonekana kuwa katika mashindano ya ubabe wa kualika na kukutana na jumbe kutoka maeneo tofauti huku kila mmoja akilenga kujijengea himaya ya kisiasa.

Profesa Kindiki ameendeleza mtindo wa mkubwa wake Rais William Ruto ambaye alipokuwa naibu rais kuelekea uchaguzi wa 2022 alitumia makazi rasmi ya mtaani Karen, Nairobi kukutana na jumbe za viongozi na wanasaisa kutoka kote nchini.

Naibu rais huyo wa tatu anaonekana kutumia mbinu sawa kujaribu kurejesha umaarufu wa serikali ambao ripoti tofauti za kura za maoni zinaonyesha umedorora.

Kwa upande wake, Bw Gachagua amegeuza makazi yake katika kijiji cha Wamunyoro kaunti Nyeri kuwa ikulu ndogo isiyo rasmi anayotumia kukutana na jumbe, wanasiasa na wataalamu wa sekta tofauti anapojiandaa kutangaza chama cha kisiasa na kutimiza ahadi yake ya kupatia eneo la Mlima Kenya mwelekeo wa kisiasa.

“Kusikiliza ni muhimu. Asubuhi ya leo, nilishauriana na Dkt Peter Mbae, aliyekuwa Mkuu wa Huduma za Utekelezaji Serikalini (GDS) katika makazi yangu ya Wamunyoro.

Mazungumzo yetu yaliacha hisia ya kudumu kwangu alipokuwa akizungumzia umuhimu wa ushirikishaji wa watu mashinani, akisisitiza kwamba mageuzi ya kweli yanaweza kutokea tu wakati sauti za raia zinasikika na kujumuishwa katika mchakato wa kufanya maamuzi.

Dkt Mbae, anayetoka Kaunti ya Nakuru, pia alinieleza maono yake wazi na kabambe ya mustakabali wa Kaunti ya Nakuru,” Bw Gachagua aliandika katika mitandao yake ya kijamii mnamo Ijumaa.

Siku hiyo, katika makazi rasmi ya naibu rais mtaani Karen, Profesa Kindiki alikutana na ujumbe kutoka Kajiado, siku mbili baada ya Gachagua kuwa mwenyeji wa ujumbe kutoka kaunti hiyo hiyo kijijini Wamunyoro

“Utekelezaji wa sera na miradi ya Serikali kwa wakati na kwa ufanisi unahitaji mashauriano ya mara kwa mara, ya makusudi na ya kina na viongozi na wadau waliochaguliwa katika sekta mbalimbali mashinani.

Uainishaji wa mipango na miradi ya maendeleo ya kupatiwa kipaumbele utafanikisha utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya mabadiliko ya uchumi, uwajibikaji na ugavi sawa wa rasilimali kwa wakati na kwa ufanisi.

Nilikuwa na kongamano la siku moja la mashauriano na viongozi waliochaguliwa, washikadau wa sekta ya uchumi na viongozi wa mashinani kutoka Kaunti ya Kajiado,” Profesa Kindiki aliandika katika kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.

Wabunge Memusi Kanchory (Kajiado ya Kati), Leah Sankaire (Mwakilishi wa Wanawake), Kakuta Maimai (Kajiado Mashariki), George Sunkuiya (Kajiado Magharibi) na aliyekuwa Gavana Dkt David Nkedianye ni miongoni mwa waliokutana na naibu rais.

Mnamo Jumatatu, wiki hii, Bw Gachagua aliupokea ujumbe kutoka Kajiado uliongozwa na Mbunge wa Kajiado Kaskazini Onesmus Ngogoyo na Seneta wa kaunti hiyo Samuel Seki.

Ulishirikisha madiwani kadhaa wa UDA na hata Mbunge wa Kajiado Kusini na Samuel Parashina aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM, Moses Konana kutoka Kajiado Magharibi.

Profesa Kindiki amesema atakutana na jumbe kutoka kaunti zote walivyokuwa wakifanya wakati wa kampeni ili kutathmini maendeleo na jinsi ya kuharakisha miradi.

Wachanganuzi wa siasa wanasema mikutano hii inalenga kushawishi viongozi wa mashinani kutomfuata Bw Gachagua.

“Kwa maoni yangu, kuna hofu kwamba viongozi wa mashinani watamfuata Gachagua ambaye amekataa kufumbwa mdomo na anaonekana kujipanga na kupata umaarufu mashinani. Kumbuka yote yalianza na Kindiki kukutana na jumbe kutoka Embu, Meru na Tharaka Nithi baada ya wakazi kuonyesha uasi kwa serikali hadi wakakataa rambi rambi za rais mashinani,” akasema mchanganuzi wa siasa Paul Bundi.

Licha ya kutokuwa na mamlaka yoyote baada ya kuvuliwa unaibu rais na nafasi yake kupatiwa Kindiki, Gachagua anaonekana kuvutia wajumbe kutoka kote nchini japo sio kubwa kama Kindiki ambaye ana madaraka na ufadhili wa serikali.

Gachagua amekutana na viongozi na wataalamu kutoka sehemu za Rift Valley, Ukambani, Kisii na Nyandarua.

Mnamo Jumatano alikutana na ujumbe wa vijana kutoka Nyanza waliotembelea kwake Wamunyoro.

Mnamo Alhamisi, Kindiki alipokuwa akikutana na viongozi waliochaguliwa kutoka kaunti ya Taita Taveta, Bw Gachagua alikuta na kundi la wataalamu kutoka kaunti ya Kilifi akiwemo Furahja Chengo, mtaalamu wa masuala ya kisiasa. Bw Bundi anasema hii ni sehemu ya ushindani kati ya Gachagua na Kindiki katika kuwania ubabe wa kinara wa Mlima Kenya.