UKEKETAJI: Juhudi zilizochangia tohara ya wanawake kupungua Afrika Mashariki
Na PAULINE ONGAJI
KULINGANA na utafiti uliofanywa na jarida la BMJ Global Health na kuchapishwa mwaka 2018, idadi ya wasichana wanaokeketwa katika kanda hii ya Afrika Mashariki imepungua katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Utafiti huu ulioangazia viwango vya ukeketaji miongoni mwa wasichana chini ya miaka kumi na minne, ulionyesha kwamba visa hivi katika eneo la Afrika Mashariki vilipungua kutoka asilimia 71.4% mwaka wa 1995, hadi 8% mwaka wa 2016.
Taifa Leo Dijitali ilizuru maeneo yanayoashiria utafiti huu ni Rombo, iliyoko kilomita 30 kutoka mji wa Loitoktok, Kaunti ya Kajiado, Kenya kutathmini hali halisi ya uovu huo.
Tangu jadi, eneo hili ambalo hasa linatawaliwa na jamii ya Wamaasai, ilikuwa kawaida kwa wasichana katika umri wa kubalehe kujiandaa kutahiriwa.
Aina ya ukeketaji uliokuwa ukitekelezwa katika eneo hili ulikuwa wa kinyama ambapo ulihusisha kuondoa huhusisha kuondoa kinembe na kinywa chote cha uke, huku sehemu hii ikisalia wazi.
Haya yote yalikuwa yakifanyika katika sehemu wazi ambapo msichana alizingirwa na wanawake waliokomaa, ambapo wawili walikuwa na jukumu la kumpanua, huku mkeketaji akiendelea na shughuli zake.
Kwa kawaida mkeketaji alijihami kwa ala zake ambazo zilihusisha aina maalum ya ngozi kwa jina Enjoni ambayo inatumika kuweka kinembe au Mouwa kama unavyotambulika kwa lugha ya Kimaasai, kabla ya kukatwa.
Aidha, awali, mkeketaji angetumia wembe maaluma wa chuma kwa jina Almoronya kwa Kimaasai. Lakini kutokana na visa vya maanbukizi ya virusi vya HIV na ili kuzingatia usafi, wembe wa kawaida ulichukua nafasi hii na sasa ndio unatumika.
Haya yote yangefanyika pasipo msichana mhusika kupewa dawa ya kutia ganzi sehemu hii kumaanisha kwamba mhusika alilazimika kuvumilia maumivu haya. Baadaye msichana angevuja na kuchukua muda mrefu kabla ya kupona.
Lakini haya yote alitarajiwa kuvumilia kwani ilikuwa ishara ya hii ingeashiria usafi na ukomavu na hivyo kuiletea boma lake fahari kuu.
Ni fahari ambayo ingejitokeza kupitia sherehe ambapo familia hata ingeua fahali huku wanawake wakiimba na kucheza densi usiku kucha, utamaduni ambao ulidhihirisha kwamba wamevuka kutoka utotoni hadi utu uzima, tayari kuozwa.
Ni suala lililongeza visa vya ndoa za mapema, na hivyo kuathiri masomo miongoni mwa watoto wasichana, huku ustawi wa eneo hili ukiendelea kuathirika.
Pia, zaidi ya yote wasichana waliokeketwa walikumbwa na hatari nyingi za kiafya zilizotokana na kuondolewa kwa sehemu hii.
Kulingana na Bi Anastacia Mashindana, 40, mwanzilishi na mwenyekiti wa kikundi cha Enduet Women group, ambacho kwa usaidizi wa shirika la Amref Health Africa, wamekuwa wakiendeleza vita dhidi ya utamaduni huu.
“Mbali na wasichana wengi waliokeketwa kusalia na makovu ya kudumu, kulikuwa na visa vya wasichana kuvuja damu hadi kufa, huku wengine wakikumbwa na matatizo ya kiafya wakati wa kujifungua,” alielezea Taifa Leo Dijitali.
Hizi ni baadhi ya sababu zilizochochea kampeni kali dhidi ya utamaduni huu uliopitwa na wakati, na cha kustaajabisha ni kwamba hata wakeketaji ambao awali walikumbwa na kibarua kigumu cha kuendeleza itikadi hizi, wakabadilika na kuwa mstari wa mbele kuokoa wasichana kutokana na ukeketaji.
Bi Rose Ndipapai, anayekisia umri wake kuwa kati ya miaka 55 na 60, ni mmoja wao. Bi Ndipapai, mkazi wa eneo la Matepes, mojawapo ya maeneo yanayojumuisha Tarafa ya Rombo, aliamua kubadilika baada ya kuwa mkeketaji kwa zaidi ya miongo miwili.
Katika tajriba yake ya zaidi ya miaka 20, kwa kawaida angetahiri kati ya wasichana 15 na 20 kwa siku. “Mara nyingi idadi hii ilitofautiana kwani kuna wakati ambapo ungeitwa katika boma la wasichana watatu, wanne au watano,” alisema.
Kulingana naye, wateja wake wengi walikuwa wazazi wa wasichana kati ya umri wa miaka 12 na 14. “Mara nyingi ni akina baba ambao wangenijia na kuniomba niwapashe tohara wanao, kwani kulingana na utamaduni wetu, watoto na hasa wa kike, ni mali ya baba. Baada ya shughuli hii mwanamume alihakikishiwa mahari nyingi ikiwa ni pamoja na mifugo na pesa,” aeleza.
Kwa Bi Ndipapai, mbali na kumletea sifa nzuri, fahari na heshima, shughuli hii ilikuwa inamhakikishia pato nzuri ambapo angehakikishiwa angaa Sh 10, 000 kutoka kwa kila familia ya msichana ambaye angepitia kisu chake.
“Kwa kila boma ambapo nilitekeleza shughuli hii, pia nilihakikishiwa makalio ya fahari huyo baada ya kuchinjwa, mojawapo ya sehemu tamu na zilizo na virutubisho vingi mwilini kulingana na utamaduni wa Kimaasai. Aidha, ningepewa bidhaa muhimu za matumizi kama vile sukari, ambapo familia yangu ilihakikishiwa kuwepo kwa chakula cha kutosha,” alisimulia.
Kwa zaidi ya miaka ishirini alitegemea kazi hii hadi mwaka wa 2011 ambapo aliamua kubadilika baada ya kupata mafunzo kuhusiana na athari za ukeketaji.
“Tulishuhudia moja kwa moja matatizo ya kiafya yaliyowakumba wanawake waliofanyiwa ukeketaji. Tungeshuhudia wanawake wakivuja damu nyingi, maumivu wakati wa hedhi na kukojoa, hatari wakati wa uja uszito kwa mama na matatizo wakati wa kuzaa kwa mtoto,” alieleza.
Bi Ndipapai ambaye ana watoto kumi anasema kwamba ni sababu hizi zilizomsukuma kuachana na shughuli hii licha ya kwamba ilikuwa inamvunia pesa nyingi.
“Nina mabinti wanne ambapo najuta kwamba watatu washakeketwa. Hii ilikuwa kabla nione mwangaza. Wa mwisho hakukeketwa na kwa sasa yuko katika kidato cha tatu,” alisema.
Ni hadithi hiyo hiyo unayoipata kutoka kwake Manangói Elemku, 50. Kwa zaidi ya mwongo mmoja, bibi huyu mama wa watoto kumi ikiwa ni pamoja na mabinti watatu, alikuwa mkeketaji stadi huku akiendesha shughuli zake katika eneo la Enduet, kilomita chache kutoka kituo cha kibiashara cha Rombo.
“Hasa nilikuwa naendesha shughuli hii wakati wa likizo za mwezi Desemba, suala lililoniletea heshima kuu miongoni mwa wanawake na wanaume,” anaeleza.
Lakini ni fahari iliyofikia kikomo baada ya kukutana ana kwa ana na masaibu ya mwanamke aliyekuwa amevuja damu nyingi alipokuwa akijifungua hasa.
“Tatizo hili kulingana na wataalam wa kiafya waliokuwa wakimshughulikia lilitokea baada ya uke wake kukosa kufunguka,” anasema.
Hii ilikuwa tu mojawapo ya matukio ambayo yalimsukuma kuacha kutekeleza ukeketaji. “Kwa bahati mbaya mabinti zangu wawili walikuwa tayari washafanyiwa ukeketaji kufikia wakati huo, lakini baada ya hayo, niliapa kamwe sitamruhusu mwingine kufanyiwa unyama huo na tayari yuko katika shule ya upili,” anaeleza.
Ni hadithi ambayo inakaribiana na ya Bi Semeiyan Sapei, 50, ambaye kwa zaidi ya miaka 15 alitembea masafa marefu kutahiri wasichana.
Bi Sapei ambaye pia msukumo wake wa kubadili mkondo ulitokana na sababu hizi, anasema kwamba changamoto kwake ilikuwa kumshawishi mumewe kwamba ukeketaji ulikuwa na madhara kinyume na dhana kwamba ilifaidi jamii.
“Kwa wanaume wa Kimaasai na hasa walio na mabinti, suala la ukeketaji sio la kujadiliwa, na hivyo hebu tafakari kibarua nilichokuwa nacho kumwambia mume wangu kwamba binti yangu aliyesalia hakuhitaji kukeketwa,” anaeleza.
Kwa upande wa Nadupoi Tipengo, 60, ambaye jukumu lake kama mkeketaji lilimpeleka katika maboma tofauti ya eneo la Enderekesi, alibahatika kwani hakuwa na kibarua kigumu kumshawishi mumewe kuhusiana na madhara ya utamaduni huu.
“Kabla ya kuona mwangaza, ningekeketa hata wasichana kumi kwa siku, lakini baada ya mafunzo haya niliamua kuachana na shughuli hii, na hata kumzuia kitinda mimba wangu asikekektwe,” aeleza.
Kwa Peninah Nekarei, 70, licha ya jukumu lake kama mkeketaji kumletea heshima sio haba, matatizo aliyoshuhudia wasichana waliokeketwa wakikumbana nayo baadaye maishani yalibadilisha mawazo yake kabisa.
Mama huyu wa watoto 12 ikiwa ni pamoja na wasichana tisa, anasisitiza kwamba kati ya mabinti zake sita waliohepuka kisu cha ngariba, hakuna atakamyeruhusu kukeketwa.
Mabadiliko haya yametokana na jitihada za chama hiki cha Enduet Women Group ambacho tangu mwaka wa 2011 kimekuwa kikiendesha kampeni dhidi ya ukeketaji katika vijiji mbali mbali katika vijiji kadha katika Tarafa ya Rombo.
Hasa wamekuwa wakielekeza jitihada zao katika mafunzo ya kusaidia wasichana na jamii kwa jumla kufahamu kuhusu masuala ya uzazi na jinsi utamaduni huu unavyowaathiri.
Kwa kawaida, wao huandaa vikao na wasichana shuleni, au hata jamii huku ujumbe wao ukiwa sio lazima wakeketwe ili kudhihirisha ukomavu wao.
“Tumekuwa tukiendesha vikao hivi katika shule za msingi na upili katika tarafa hii huku tukihimiza jamii kumakinika na elimu ambapo kauli mbiu yetu kwa sasa ni ‘kutahiri ubongo’,” asema.
Na matokeo yao yamehisiwa katika eneo la Rombo ambalo limeendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya wasichana wanaojiunga na shule za upili na vyuo vikuu.
Bw Boniface Mutembei, Naibu Kamishna wa kaunti katika Tarafa ya Rombo, anasema kwamba ameshuhudia ongezeko la idadi ya wasichana katika shule za upili kutoka 1000 tangu alipochukua hatamu Agosti mwaka wa 2016, hadi 2000 mwaka 2018.
“Kwa upande mwingine idadi ya wanafunzi wasichana wanaojiunga na vyuo vya upili katika eneo hili imeongezeka kutoka 60 hadi 300 kwa sasa,” anasema.
Lakini hata jamii hii inapozididi kufurahia matokeo hayo, kuna hatari kwamba huenda wakeketaji hawa wakarejelea shughuli zao za awali. Baada ya kuachana na utamaduni huu, wanawake hawa wanakumbwa na vishawishi vya kurejelea kazi hii.
“Awali tulikuwa tuaunda pesa nyingi kutokana na kazi hii, na sasa tunakumbwa na umaskini wa ajabu ambapo tumelazimika kufanya kazi za sulubu kama vile kulimia watu shambani, na wakati mwigine kuuza mboga, na hivyo kupata angaa Sh 300 kila siku, pesa ambazo hazitoshi,” alieleza Bi Ndipapai.
Kulingana na Mashindana, iwapo hatua kabambe hazitachukuliwa kuwasaidia wakeketaji hawa wa zamani kuweza kujitegemea kiuchumi, basi ndoto hii itazimwa.