Mswada waundwa kudhibiti ‘beach boys’ baada ya watalii kulalamika kuwa wanakera
WADAU wa sekta ya utalii katika Kaunti ya Kwale wameanza kutayarisha Mswada wa Usimamizi wa Fuo za Kwale ili kuhakikisha kuna usalama na usafi kwa madhumuni ya kustawisha sekta hiyo.
Wadau hao kwa muda wamekuwa wakilalamikia kero kutoka kwa vijana wanaoendeleza huduma mbalimbali ufuoni, almaarufu kama beach boys, ambapo baadhi yao hudaiwa kujihusisha na uhalifu.
“Mara tu tutakapotunga sheria hii, tutakuwa na utaratibu ufukweni,” alisema Mwenyekiti wa Wahudumu wa Utalii Pwani Kusini, Bi Sally Mathenge.
Polisi walithibitisha huwa wanapokea ripoti za unyanyasaji wa watalii katika ufuo wa Diani, lakini kesi hizi zimepungua katika miezi michache iliyopita.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Polisi wa Kitengo cha Watalii cha Diani, Bw Godfrey Parteneu, visa vya unyanyasaji vimekuwepo.
Hata hivyo, alisema maonyo ya mara kwa mara, pamoja na elimu kwa wahudumu wa ufuoni, yamepunguza malalamishi ya watalii.
“Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, tumeona kesi hizi zimepungua lakini sio asilimia 100. Tunahakikisha kwamba wahudumu wote walio kando ya ufuo wanajiunga na vikundi vilivyoteuliwa ili kusaidia kufuatilia visa vyovyote vya unyanyasaji na hili limefanya kazi,” alisema Bw Parteneu.
Wadau wa utalii sasa wanatumai kuwa mswada unaotungwa ukipitishwa kuwa sheria, utasaidia kudhibiti shughuli za ufuoni kwa kuhakikisha kuna usalama kwa watalii.
Afisa Mtendaji wa Chama cha Wahudumu wa Hoteli nchini (KAHC), tawi la Pwani, Dkt Sam Ikwaye, alisema imechukua zaidi ya miaka kumi kuanzisha kanuni za ufuoni.
Kulingana naye, mara nyingi mchakato huo huingiliwa na masuala ya siasa. Hii ni kutokana na wanasiasa ambao hutaka kuonekana wanatetea maslahi ya vijana.
Dkt Ikwaye alisema takwimu za awali za Bodi ya Utalii ya Kenya (KTB) zilionyesha kuwa watalii 7 kati ya 10 walisema hawakufurahishwa na ziara yao katika Pwani ya Kenya kutokana na usumbufu.
“Tunataka kanuni hizi ziwe sehemu ya sheria katika Kaunti ya Kwale. Usimamizi wa ufuo umegatuliwa lakini miaka hii yote hakuna serikali ya kaunti iliyoweka sheria za kulinda fuo ambazo zina jukumu muhimu kwa uchumi wa eneo la Pwani,” alisema.
Aliongeza kuwa, hatua hii pia itakuza uwajibikaji kwa baadhi ya wawekezaji ambao wanajulikana kuchafua fuo kwa kutupa taka ovyo.
Maoni yake yaliungwa mkono na Meneja Mkuu wa Hoteli ya Leopard Beach Kioko Musyoki, ambaye alisema wadau walipaswa kuchukua hatua ili kuhakikisha Diani inaendelea kupigiwa kura kama ufuo bora zaidi barani Afrika.
“Wengi wanasema ufuo ni safi lakini ‘beach boys’ huishia kuwa kero,” akasema.