Ndoa ya ANC na UDA baraka kwa Gachagua
MOJAWAPO ya vipengele katika sheria kuhusu miungano ya vyama vya kisiasa, ikiwa ni pamoja na wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto na Amani National Congress (ANC) kinachohusishwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, huenda kikafanya Magavana,Wabunge na Madiwani kuhama,Taifa Leo inafichua.
Kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa ambacho kinaeleza masharti ya vyama kuungana, kinaeleza kwamba viongozi waliochaguliwa – ambao wanapinga vyama vilivyowadhamini kuungana- wana uhuru wa kuhamia vyama vingine vya kisiasa au kuwa huru.
“‘Pale ambapo vyama vinaungana chini ya kifungu hiki, mwanachama wa chama cha siasa ambacho kinaungana na chama kingine cha siasa atachukuliwa kuwa mwanachama wa chama kipya cha siasa,” kinaeleza kifungu hicho cha sheria ya vyama vya kisiasa.
“Mwanachama ambaye ni Rais, Naibu Rais, Gavana au Naibu Gavana, Mbunge au Mwakilishi katika Bunge la Kaunti, na ambaye hataki kuwa mwanachama wa chama kipya cha kisiasa kilichosajiliwa baada ya kuunganishwa, ataendelea kuhudumu katika ofisi aliyochaguliwa kwa muda uliosalia, na anaweza kujiunga na chama kingine cha siasa au kuchagua kuwa mwanachama huru ndani ya siku thelathini baada ya kusajiliwa kwa chama kipya,” inaeleza sheria.
Kifungu hiki kinaweza kutumiwa na washirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhama UDA, hasa wale wanaotoka eneo la Mlima Kenya.Hivi majuzi, Bw Gachagua alitangaza mipango ya kuzindua chama chake kipya cha kisiasa, ambacho kinaweza kunufaika na kifungu hiki cha sheria ya vyama vya kisiasa.
Baadhi ya viongozi waliochaguliwa kutoka eneo la Mlima Kenya wameanza kuungana na Bw Gachagua baada yake kutimuliwa serikalini.Hata hivyo, wamekuwa waangalifu, wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kwenda kinyume na msimamo wa UDA.
Baadhi ya washirika wa Bw Gachagua waliambia Taifa Leo kwamba wanasubiri cheti cha usajili baada ya UDA na ANC kuungana kabla ya kuhama chama tawala.Kuhama kwao kwa wingi kunaweza kuwa na athari kubwa za kisiasa, ikiwa ni pamoja na kubadilisha miungano ya walio wengi na walio wachache katika Bunge la Kitaifa na Seneti.
Pia, unaweza kunyima UDA mamilioni ya pesa za Hazina ya Vyama vya Siasa, ambazo hugawanywa kulingana na idadi ya viongozi waliochaguliwa kutoka kila chama.Kwa sasa, UDA inapokea kiasi cha juu zaidi kutoka hazina ya vyama vya kisiasa.
Katika mgao wa hivi punde wa Sh1.2 bilioni, UDA ilipata Sh558.49 milioni, ikifuatwa na ODM kwa Sh298.3 milioni.Kwa sasa Kenya Kwanza ndio muungano wa walio wengi kutokana na idadi kubwa ya wabunge wa UDA, ambao wengi wanatoka Mlima Kenya, ngome ya Bw Gachagua na Bonde la Ufa anakotoka Rais Ruto.
Kenya Kwanza ina wabunge 179 katika Bunge la Kitaifa dhidi ya 157 wa muungano wa Azimio La Umoja One wa Kenya.Kifungu hicho pia kinaweza kumuumiza Bw Mudavadi ikiwa baadhi ya wanachama wake wa ANC watakataa kujiunga na UDA.UDA bado haijapenya Magharibi, eneo ambalo ni ngome ya ODM.
Taifa Leo iliwasiliana na Msajili wa Vyama, Bi Ann Nderitu kuhusu maana ya kifungu hicho.Hata hivyo, hakujibu maswali yetu moja kwa moja lakini alituelekeza kusoma Kifungu cha 11 cha Sheria kinachozungumzia miuungano.’Tafadhali soma Kifungu kizima cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa,’ alisema Bi Nderitu.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa ANC, Bw Omboko Milemba, aliambia Taifa Leo kwamba wanafahamu maana ya kifungu hicho.Bw Milemba alisema wamechukua tahadhari zinazofaa kuwazuia wapinzani wao kutumia kifungu hicho kukihujumu chama tawala.“Sheria ni kama ulivyoisoma, na ninaweza kukuambia kwamba tumechukua tahadhari. Ni sheria, tuko tayari na tumeishughulikia,” akasema Bw Milemba, ambaye alikataa kufafanua.
Kwa mujibu wa Sheria, chama cha siasa kinaweza kuungana na chama kingine cha siasa na kuunda chama kipya cha siasa au kumezwa na chama ambacho tayari kimesajiliwa.Mtaalamu wa Masuala ya Katiba, Bobby Mkangi alisema sheria hiyo inafungulia milango wanachama wasioridhika kuhama na kujiunga na vyama vingine vya kisiasa bila kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA