Jamvi La Siasa

Khalwale, Echesa wakaba koo Barasa kuhusiana na matumizi ya Sh35 bilioni

Na SHABAN MAKOKHA February 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UHASAMA wa kisiasa unaendelea kushuhudiwa Kaunti ya Kakamega baada ya baadhi ya viongozi kumtaka Gavana Fernandes Barasa afafanue jinsi ambavyo ametumia Sh35 bilioni ambazo kaunti hiyo ilitengewa tangu 2022.

Hii ni baada ya kubainika kuwa miradi mingi imekwama. Viongozi hao wakiwemo Seneta Boni Khalwale, mbunge wa Matungu Peter Nabulindo na waziri wa zamani Rashid Echesa wamesema uongozi wa Bw Barasa haujafaa wakazi wa Magharibi.

Watatu hao wanadai raia wamekuwa wakikosa mahitaji ya kimsingi hasa kwenye sekta ya afya ambayo inaelekea kuporomoka. Wanadai hospitali nyingi hazina dawa na wakazi hawajakuwa wakipokea huduma bora za afya.

Bw Khalwale alisema mgao kutoka kwa serikali haukuwa ukiwanufaisha wakazi wakidai pesa zimekuwa zikifujwa na utawala wa Bw Barasa.

“Pesa zimekuwa zikifikia kaunti kupitia bunge la seneti na Kakamega imetengewa pesa za kutosha. Mwaka wa kwanza tulipokezwa Sh17 bilioni na mwaka huu tumepata Sh18.5 bilioni.

“Hata hivyo, barabara ziko katika hali mbaya na hospitali hazina dawa wala wananchi hawahudumiwi vyema,” akasema Bw Khalwale.

Seneta huyo pia alilalamika kuwa utawala wa Bw Barasa umeanza kubagua baadhi ya maeneo katika uajiri na pia miradi inayotolewa na kaunti.

Kiongozi huyo alikuwa akiongea kwenye wadi ya Chevaywa, eneobunge la Lugari ambako aliahidi kuwa ataendelea kusukuma kaunti itoe nafasi zote za uajiri na miradi kwa usawa.

Bw Nabulindo naye alitoa mfano wa soko la kisasa la Koyonzo ambalo ujenzi wake umekwama tangu 2021 na sasa wafanyabiashara wamehamishiwa kwenye barabara ya Mumias-Busia kuendeleza biashara zao.

Alilalamika kuwa wafanyabiashara hao sasa wamejiweka hatari kuhusika kwenye ajali ya barabarani. Vilevile alilalamika kuwa wagonjwa ambao wanatembelea Hospitali ya Kaunti Ndogo Matungu wanalazimika kununua dawa na sindano pamoja na vifaa vingine vya kimatibabu.

Wikendi mbunge huyo alivurugana na Bw Barasa akisema maisha yake yako hatarini baada ya kupokea vitisho kutoka kwa gavana.

“Ametishia kuwa atanitimua Matungu mahali ambapo nilizaliwa na kuhakikisha kuwa sipo. Hata hivyo, sitapiga ripoti kwa polisi kwa sababu nami nina njia ya kujilinda na haitampendeza,” akasema Bw Nabulindo.

Viongozi hao sasa wanawataka madiwani wa kaunti wamtimue Bw Barasa mamlakani.

Bw Echesa alisema Bw Barasa amekuwa akitumia pesa nyingi kuwakodisha wahuni pamoja na kuwalipa wafuasi wake wamshangilie kwenye hafla za umma pamoja na mazishi.

Alisema lau pesa hizo zingekuwa zikitumia kwenye miradi ya maendeleo, kaunti ingekuwa imepiga hatua kubwa.

Bw Echesa pia aliwashutumu madiwani kwa kutomakinikia majukumu yao na badala yake kugeuaka vibaraka wa Bw Barasa.

Akizungumza alipotembelea soko la Harambee, Bw Barasa alimkemea Bw Nabulindo akisema hajafanya lolote la maana kimaendeleo na amegeuka diwani wa kuchunguza utendakazi wa serikali ya kaunti.

“Maendeleo kwenye eneobunge hili yapo chini na mbunge haoni hilo. Ukienda maeneobunge mengine ghorofa zimejengwa na maendeleo yanaonekana lakini hapa Matungu hakuna chochote.

“Hapa amekanyaga nyaya yenye umeme na nikimtokea, hataipenda,” akasema.

Bw Barasa amewalaumu wapinzani wake kwa kutoona miradi mingi inayoendelea katika gatuzi hilo kwa sababu wanamakinika tu kumwondoa mamlakani mnamo 2027.