Maoni

MAONI: Kenya itavuna pakubwa kutokana na ziara aliyofanya Rais nchini Misri

Na JACKTONE NYONJE February 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ILIKUWA mojawapo ya ziara zilizolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Kenya na Misri.

Mataifa haya mawili yana usemi na umuhimu mkubwa wa kijiografia katika bara la Afrika.

Baada ya Rais William Ruto kukutana na mwenyeji wake Rais Abdel Fattah El-Sisi, mikataba 12 ilitiwa saini.

Mikataba iliyoazimia kuimarisha biashara baina ya Misri na Kenya, uwekezaji, ushirikiano katika elimu na utafiti pamoja na ubadilishanaji wa teknolojia baina ya mataifa haya.

Uhusiano baina ya Misri na Kenya una historia ndefu. Misri ilianza kutagusana kibiashara na pwani ya Afrika takriban miaka 3000 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristu.

Hata wakati Kenya ilipokuwa katika vita vya ukombozi kujinasua kutoka kwa ukoloni wa Muingereza, Misri ilitoa mchango mkubwa kupitia rais wake Gamal Abdel Nasser ambaye alilipigia upatu suala la MauMau katika majukwaa mengi na vilevile kuwaalika mara kwa mara mashujaa wa ukombozi kutoka Kenya kama vile Jomo Kenyatta, Oginga Odinga, Tom Mboya, Joseph Murumbi, James Gichuru miongoni mwa wengine.

Si hayo tu hata baada ya uhuru, Misri ilizidi kuipiga jeki Kenya katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kuviimarisha vikosi vya ulinzi na usalama vya Kenya kupitia kwa kutoa mafunzo mbalimbali.

Kibiashara, Misri ni miongoni mwa wanunuzi wakuu wa chai ya Kenya. Inakisiwa Kenya huuza yapata kilo 84 milioni za chai kila mwaka zenye pato la bilioni 21.

Misri imepiga hatua katika nyanja mbalimbali zikiwemo kilimo, uzalishaji wa viwandani, elimu ya juu na utafiti, diplomasia, michezo, matumizi ya rasilimali ya maji, teknolojia ya mawasiliano, utamaduni na lugha, usawa wa kijinsia na uhusishwaji wa vijana katika ustawi wa kitaifa, uhifadhi wa ustaarabu wa kale kama turathi ya kitaifa miongoni mwa maendeleo mengine.

Sasa hivi Kenya inakabiliwa na changamoto ya kizazi cha Gen-Z ambacho kinalalamikia kubaguliwa katika maamuzi na ushirikishwaji katika maendeleo ya taifa.

Kenya inaweza kujifunza na Misri jinsi inavyowakuza vijana wake kupitia muungano na jukwaa la Harakati ya Nasser ambao hutoa fursa kwa vijana wa jinsia zote kuvinoa vipawa vyao, hivyo kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Aidha, Kenya inaweza kujifunza namna ya kuendeleza kilimo katika sehemu kame kupitia teknolojia ya unyunyiziaji maji.

Misri ni miongoni mwa waasisi wa teknolojia hii duniani ambapo wanendeleza kilimo kwa kutegemea maji ya Mto Nile.

Kenya na Misri zinaweza kushirikiana katika kutunza maziwa makuu pamoja na vyanzo vyake.

Uwekezaji katika kuvitunza vyanzo hivi pamoja na kuwahamasisha raia wote wa mataifa ya ukanda huu ni muhimu sana.

Aidha, umuhimu wa kuwekeza katika lugha hususan katika Kiswahili na Kiarabu kutachangia sana katika kupanua mawasiliano na kuleta mshikamano zaidi baina ya mataifa haya.

Na muhimu kwa mataifa haya kutumia ushawishi wao katika kudumisha umoja na uwiano katika bara la Afrika maana maendeleo huendana na mazingira ya amani.

-Jacktone Nyonje ni Mkurugenzi wa Mafunzo wa tume ya IEBC