Jamvi La Siasa

Gachagua sasa adai alipewa Sh2 bilioni ajiuzulu akazikataa

Na RUSHDIE OUDIA February 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua, amedai kuwa Rais William Ruto alijaribu kumpa Sh2 bilioni na tunu nyingine ili ajiuzulu badala ya kusubiri kuondolewa na bunge mnamo Oktoba mwaka jana.

Bw Gachagua alisema licha ya kushawishiwa kwa hela, kupewa ulinzi, mshahara na mwanya wa kuwania kiti cha kisiasa baadaye, alisimama wima na kukosa kujiuzulu.

Hata hivyo, alisema kuwa katiba iko wazi kuwa mtu akiwa na kesi inayoendelea mahakamani, hawezi kuzuiwa kuwania wadhifa wa kisiasa.

“Sina ubinafsi kwa hivyo hata nisipowania, hakuna tatizo. Iwapo ningekuwa mtu wa tamaa, ningeridhia zawadi za Rais na kujiuzulu,” akasema Bw Gachagua.

“Hata hivyo, nilijiuliza iwapo adui anaweza kukupa tunu na ahadi zote hizi, kwa sababu mara nyingi wanaokuchukia, hupanga jinsi ya kukuangusha,” akaongeza.

Bw Gachagua alikuwa akiongea kwenye mahojiano na idhaa mbalimbali zinazotangaza kwa lugha ya Kiluhya.

Wakati wa mahojiano hayo, alisema si lazima awanie ila mnamo Disemba mwaka ujao, atamtangaza mwanasiasa ambaye atamenyana na Rais Ruto mnamo 2027.

Kiongozi huyo ambaye amewahi kuhudumu kama mbunge wa Mathira, alionya eneo la Magharibi dhidi ya kuhadaiwa na kuunga mkono Rais Ruto mnamo 2027.

“Shida yenu watu wa Magharibi ni kushiriki meza ya majadiliano mkiwakilishwa na Raila Odinga badala ya viongozi wenu. Kama jamii ambayo ina wapigakura wengi na ya pili nchini, jiamulieni mambo yenu badala ya kumtegemea Raila,” akasema Bw Gachagua.

Licha ya dhana kuwa siasa haina uadui wa milele, aliyekuwa naibu rais aliondoa kabisa uwezekano wowote wa kushirikiana na Rais katika maisha yake ya kisiasa.

Alikuwa akirejelea matamshi ya mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, kuwa kuna uwezekano wa viongozi hao wawili kushirikiana baadaye siasani. Bw Gachagua alisema Mlima Kenya ushaondoka serikalini na hakuna nafasi yoyote ya kurudi.

Mwezi uliopita, Rais Ruto akiwa Magharibi, aliwaambia wapinzani wake wasahau kuwa watamwangusha debeni mnamo 2027.

Hata hivyo, Bw Gachagua alijinaki kuwa ana mpango mahususi ambao utahakikisha upinzani unamshinda Rais kwa kura milioni sita huku wakilenga kura milioni 15.

“Hata Uhuru na Raila walisema hivyo 2022 na tukawashinda. Atashangaa, tutamshinda asubuhi na mapema,” akasema.

Katika eneo la Magharibi, Bw Gachagua analenga kushirikiana na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa na aliyekuwa Katibu wa UDA Cleophas Malala. Katika upande wa Rais Ruto wapo Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla.

Bw Gachagua aliambia jamii ya Mulembe kuwa umoja wao ndio utawasaidia kupata uongozi wa nchi.

“Jamii ambayo imeungana ni tishio kwa Rais Ruto ndiyo maana anapigana na wale wanaopinga ajenda yake ya kugawanya jamii,” akasema.

Vilevile alionya dhidi ya hatua yoyote ya kuwashawishi madiwani wamtimue Gavana Natembeya uongozini, akisema hilo litasababisha pengo la uongozi kwenye gatuzi hilo.

Bw Gachagua alisema Rais analenga Magharibi na kutumia ujanja wake kuwahadaa wamuunge mnamo 2027 baada ya kufahamu amepoteza Mlima Kenya.

Kwa Mabw Mudavadi na Wetangúla, Bw Gachagua aliwataja wawili hao kama viongozi waoga na akawataka wamshinikize Rais atekeleze yaliyomo kwenye mkataba walioutia saini mnamo 2022.

“Aliwaahidi kilomita 1000 za barabara. Iwapo Magharibi ingekuwa na kiongozi ambaye si mwoga na anawapenda watu wake, yaliyokuwepo kwenye mkataba wa 2022 yangekuwa yametimizwa,” akasema.