Mwanamfalme na kiongozi wa kiroho wa Shia Ismaili The Aga Khan afariki
MWANAMFALME Karim Al-Hussaini Aga Khan wa IV, Imamu wa 49 wa Waislamu wa Shia Ismaili na Mwenyekiti wa shirika la kimaendeleo la Aga Khan Development Network (AKDN), ameaga dunia.
Taarifa kutoka kwa Diwan wa Ismaili inasema kwamba The Aga Khan alifariki jijini Lisbon, Ureno, akiwa na umri wa miaka 88, na alikuwa amezingirwa na familia yake.
“Katika maisha yake yote, akiwa kiongozi wa kidini, alifunza kwamba uislamu ni imani inayofunza upole, uungwana, kuvumiliana na kudumisha heshima kwa kila binadamu,” ikasema taarifa hiyo.
Kufikia kufariki kwake, juhudi za Aga Khan zilikuwa zimefungamana kwenye nyanja nyingi za kimaisha, haswa Kenya, ambako jina lake lipo kwenye taasisi nyingi ambazo zinaendelea kubadilisha maisha.
Kuanzia kwa The Aga Khan Schools, The Aga Khan University Hospital na vituo vyake vingi vya kimatibabu, wameweka kipau mbele utoaji huduma bora.
Kupitia kwa Aga Khan Development Network (AKDN), uwepo wake unasikika kupitia uwekezaji katika shirika la Nation Media Group, Industrial Promotion Servives, Allpack Industries, Farmer’s Choice, Premier Food Industries na idara ya utalii vilevile.
Habari zaidi zitafuata…