Habari

Amri ya Ruto ya kutoa vitambulisho bila kupiga msasa wakazi mpakani yazua maswali

Na MANASE OTSIALO February 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HATUA ya kupiga marufuku kuwapiga msasa wakazi wa eneo la Kaskazini Mashariki wanaotuma maombi ya kupata vitambulisho vya kitaifa itasababisha madhara zaidi kuliko manufaa kwa Wakenya, wataalam wa usalama wameonya.

Wataalam wamefafanua haja ya kuwapiga msasa wanaojisajili kabla ya kutoa vitambulisho vya kitaifa ilichipuka kutokana na hali ya raia wa kigeni kufurika nchini.

Mtaalam wa masuala ya kiusalama George Musamali, ametaja tangazo la Rais William Ruto kuwa la kisiasa linalolenga uchaguzi mkuu wa 2027.

Alisema uamuzi huo unanuiwa kusajili idadi kubwa iwezekanavyo ya wapiga kura kutoka Kaskazini mwa nchi.

Akiwa Kaunti ya Wajir katika ziara yake ya pili kukagua maendeleo, Rais Ruto alitangaza kufutilia mbali mchakato wa kuwapiga msasa wakazi eneo hilo wanaotafuta vitambulisho vya kitaifa.

Kulingana na Rais Ruto, watoto wote Wakenya ni sawa kuambatana na Katiba 2010 na hakuna eneo linalofaa kubaguliwa kuhusiana na maombi ya kupata stakabadhi hiyo muhimu.

“Nataka kuwahakikishia ubaguzi ulioshuhudiwa sehemu hii kwa miaka 60 iliyopita utafika kikomo. Wakati mtoto kutoka Mandera, Wajir au Garissa anapotuma maombi ya kitambulisho na kuulizwa maswali tele, si sawa na ni sharti suala hili likome kuanzia sasa,” alisema Rais.

Akiwa kwenye uwanja mashuhuri wa Orahey, mjini Wajir, Ruto alisomea umati tangazo hilo.

Alisema wakazi wa kaunti zilizo mipakani wamekuwa kihistoria wakipatiwa masharti ya ziada yanayohusu mchakato wa kuwapiga msasa ili wapatiwe vitambulisho vya kitaifa.

Mchakato huo umekuwa hujuma, usio wa haki na unaowabagua Wakenya wanaoishi mipakani, alisema.

Aliagiza msajili wa watu kuendelea kubatilisha masharti na michakato kuhakikisha kuwepo usawa, haki na uwazi.

“Tumekabiliana na ubaguzi kwa miaka mingi nchini. Mchakato wa upigaji msasa uliwafanya vijana wetu kuonekana kama wasio Wakenya kwa sababu ya maswali chungu nzima,” alisema.

“Ninatangaza na kuamuru kwamba, masharti ya ziada na ubaguzi wa kikabila ambayo wakazi wa kaunti za mipakani hupitishiwa yamekoma kuanzia sasa.”

Alisema ametimiza ahadi aliyotoa akifanya kampeni kwa kufutilia mbali mchakato wa upigaji msasa kuhusu vitambulisho vya kitaifa.